27 August 2012
DC Lushoto ahadharishwa na wananchi
Na Yusuph Mussa, Lushoto
BAADHI ya wakazi wa Kata ya Vuga, Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga, wamesema Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw.Majjid Mwanga hatafanikiwa kuzuia uharibifu wa mazingira na uvunaji haramu wa mazao ya misitu, kama wenyeviti na watendaji wa vijiji katika kata hiyo wataendelea kubaki madarakani.
Wakazi hao waliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Kihitu na kushirikisha wakazi wa vijiji nane ambao walikwenda kijijini hapo kuziba mashimo ya madini kwenye chanzo cha maji Nkindo.
Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na Bw.Mwanga, mkazi wa kijiji hicho, Bw. Abdulsalam Manandi, alisema wanaochangia kuharibu mazingira ni wenyeviti na watendaji wa vijiji kuruhusu uchimbaji madini na kukata magogo katika Msitu wa Ndelemai.
“Mkuu wa Wilaya kama watendaji na wenyeviti wa vijiji hawatawajibishwa kwa kuondolewa madarakani, uharibifu wa vyanzo vya maji na ukataji wa miti katika msitu huu utaendelea hivyo kukuharibia na wewe mwenyewe,” alisema Bw.Manandi.
Kwa upande wake, Bw.Mwanga alisema jukumu la kuwatoa viongozi hao madarakani lipo kwa wananchi wenyewe kwa kuitisha mikutano ya kijiji na kuwapigia kura ya kutokuwa na imani nao.
“Sitakubali kuona vyanzo vya maji vikichezewa hata kama vina madini au kufanya shughuli za kilimo pembezoni mwa maji, pia kuna watu wanakata magogo, nawahakikishia tutavunja mtandao wa wezi wa mazao ya misitu,” alisema Bw.Mwanga.
Ofisa Misitu wilayani hapa, Bw.Rashid Hassan, alisema wananchi wanapaswa kufanya shughuli za kilimo mbali na vyanzo vya maji kwa kuacha mita 150 za mzunguko katika vyanzo hivyo na mita 45 kwenye njia ya maji.
Diwani wa kata hiyo, Bw.Ali Sechonge, aliomba radhi kwa Bw.Mwanga na kudai hawatarudia kuruhusu wachimbaji madini kuvamia eneo hilo na kuleta usumbufu kwa wananchi na viongozi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment