22 August 2012

FRAT yawapitisha akika Kisiwa



Na Janath Abdulrahimu

WAGOMBEA watatu kati ya watano waliowsilisha rufani zao katika Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Waamzi nchini (FRAT), wamerejeshwa katika nafasi walizoomba kwenye uchaguzi uliosimamishwa na Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) mwaka 2010.


Akizungumza Dar es salaam jana Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Muhidin Ndolanga alisema wagombea waliorejeshwa katika nafasi hizo ni Hamisi Kisiwa (Mwenyekiti), Sijali Mzeru na Jovin Ndimbo.

Alisema wagombea ambao hawakurejeshwa ni Israeli Nkongo na Kennedy Mapunda, ambao wote ni waamuzi na kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, wanatakiwa kustaafu nafasi hizo kwanza.

Ndolanga aliwataka viongozi wa mikoa kutuma majina ya viongozi wapya kwa Kamati ya Uchaguzi chama hicho na ikidhihirika viongozi waliochaguliwa ni waamuzi, uchaguzi wa viongozi hao watakuwa batili na hawatashiriki katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi.

Aliwataka waamuzi wastaafu wanaotaka kujitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za FRAT kuanzia Agosti 21, mwaka huu na mwisho wa kurejesha fomu hizo itakuwa Agosti 27, kabla ya kufanyika uchaguzi 30 Septemba mwaka huu.

Alisema fomu zitalipiwa ada kufuatana na nafasi ya mgombea ambapo Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Mkuu Msaidizi na Mhazini watatakiwa kulipia sh. 200,000 kila mmoja.

Ndolanga alisema Mjumbe wa kuwakilisha FRAT kwenye Mkutano wa TFF, Mjumbe wa kuwakilisha waamuzi wanawake na Wajumbe watatu, waliochaguliwa na Mkutano Mkuu kuingia katika Kamati ya Utendaji watalipia sh. 100,000 kila mmoja.

No comments:

Post a Comment