28 August 2012

CCM: Hatuiombi radhi CHADEMA *Nape asisitiza ushahidi wa kutosha upo *Wajipanga kumfikisha Dkt. Slaa kortini



Na Salim Nyomolelo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewataka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwenda mahakamani haraka badala ya kusubiri kuombwa radhi ili kusafishwa dhidi ya madai ya chama hicho kupewa fedha na mataifa tajiri.


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi ya CCM, Bw. Nape Nnauye, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema CCM inao ushahidi wa kutosha kuhusu madai hayo dhidi ya CHADEMA na wapo tarayi kutoa uthibitisho huo mahakamani badala ya kuomba radhi kama wanavyotaka.

Bw. Nnauye alisema viongozi wa CHADEMA wameshindwa siasa badala yake wameamua kufanya utabiri na kumtaka Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Willibrod Slaa, kuiomba radhi CCM na kama atashindwa kufanya hivyo watamburuza mahakamani.

“Tutamburuza mahakamani na kumdai fidia ya sh. bilioni tatu pamoja na shilingi moja, kwa tuhuma za kusema uongo kuwa CCM imeingiza silaha kutoka nje ya nchi tena bila kulipia ushuru.

“Jana (juzi), CHADEMA walinitaka niombe radhi au wananipeleka mahakamani na kudai fidia ya sh. bilioni tatu, wakidai mimi nimesema chama chao kinapata mabilioni ya fedha kutoka kwa mataifa tajiri, mkubwa hatishiwi nyau, nawataka waende haraka mahakamani wala wasisubiri hizo siku saba,” alisema.

Alisema CCM ina ushshidi wa kutosha kuhusu madai aliyotoa hivyo kama wataenda mahakamani itapendeza zaidi maana huko ndiko pazuri kutoa uthibitisho kuhusu madai yake.

“Niwahakikishieni kama tukithibitisha na Msajili wa Vyama vya Siasa, akapata uthibitisho huo, chama chao kinafutwa” alisema Bw. Nnauye na kuongeza kuwa, tayari ameshawaagiza wanasheria wa chama hicho kuandaa barua ya kusudio la mashitaka hayo.

Bw. Nnauye alikiri kupokea barua kutoka CHADEMA ya kumtaka kuomba radhi ndani ya siku saba na kulipa fidia ya sh. bilioni tatu.

“Sipo tayari kuiomba radhi CHADEMA, bali CCM inatoa siku saba kwa Dkt. Slaa atuombe radhi,” alisema Bw. Nnauye.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari Bw. Nnauye alisema kuwa wameamua kulipwa fidia ya sh. bilioni tatu na shilingi moja ili isifanane na madai yao ya bilioni tatu.

Wakati huo huo, CHADEMA kupitia Mkurugenzi wake wa Habari na Uenezi, Bw. John Mnyika, alisema kwa sababu CCM kimeshindwa kujibu hoja zao, watakiburuta mahakamani.

“CCM inatoa vioja badala ya kujibu hoja zetu za msingi, Dkt. Slaa alitaja hadi namba ya silaha hivyo wao walipaswa kutoa maelezo, katika uchaguzi mdogo wa Igunga, mkoani Tabora, Katibu Mkuu wa chama hiki alidai CHADEMA tuliingiza magaidi kutoka nje ya nchi jambo ambalo walishindwa kulithibitisha,” alisema.

Akizungumzia hoja ya CHADEMA, kupoteza mvuto wa chama iliyotolewa na Bw. Nnauye, alisema suala hilo liachiwe wananchi.

Juzi Bw. Mnyika aliitaka CCM kuomba radhi pamoja na kulipa fidia ya sh. bilioni tatu kwa kukituhumu chaoa chao kuwa kinawarubuni wananchi na kuchangisha fedha wakati kikipokea mabilioni ya fedha kutoka kwa wafadhili.

1 comment:

  1. nape oyeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee

    ReplyDelete