28 August 2012
DC apoteza msafara wa Mwenge
Na Salma Mrisho, Geita
KATIKA hali isiyo ya kawaida, mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Geita, juzi ziliingia dosari baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Manzie Mangochie, kuupoteza msafara wake.
Hali hiyo ilikwamisha ukaguzi wa miradi iliyokuwa ikaguliwe na Kiongozi wa mbio hizo kitaifa, Kapteni Honest Mwanossa.
Msafara huo ulikwama kwa dakika 10 katika Kijiji cha Ngula, Kata ya Nyakagwe, ambapo kitendo hicho kilimkera kiongozi wa mbio hizo na kutoa kalipio kali kwa Mangochie, ambaye pia ndie Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Miradi iliyoshindwa kukaguliwa ni pamoja na ule wa Kikundi cha Kuweka na Kukopa cha Nyamalimbe.
Kapteni Mwanossa aliaonekana kusikitishwa na tukio hilo hata kushindwa kutoa hutuba kwenye uzinduzi wa mradi wa shamba bora la mbegu za muhogo ambayo ilisomwa na msaidizi wake, Kadia Godfrey.
“Kilichoniuma zaidi wingi wa wananchi waliokuwa wakisubili mwenge katika mradi tulioshindwa kuukagua, huu ndio mwanzo wa wananchi kuichukia Serikali yao,” alilalamika kiongozi huyo.
Dosari nyingine ilitokana na Mkuu huyo wa Wilaya kukabidhi Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bw. Moses Minga, risala ya Wilaya nyingine ili aweze kuisoma.
Wakati Bw. Minga akisoma risala hiyo, alilazimika kusimama kwa muda baada ya kubaini kuwa, ilikuwa taarifa jirani sio ya Geita na kueleza kuwa, taarifa hiyo ilikuwa ya Nyang’hwale, wakati mwenge huo ukiwa tayari umeanza kupewa heshima.
“Mkuu wa Wilaya hii taarifa ni ya Nyag’hwale, sio ya Geita, risala husika iko wapi,” aliuliza Bw. Minga, ambapo Mkuu wa Wilaya alipasa sauti mbele ya wananchi kumuita dereva wake ili aweze kumpelekea taarifa hiyo.
Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya mwenge huo kufika kwenye Kijiji cha Nyakagwe kwa ajili ya mkesha. Kiongozi wa mbio hizo alifungua miradi mbalimbali ikiwemo ya afya pamoja na Kituo cha Polisi kilichojengwa kwa nguvu za wananchi na halmashauri.
Katika hotuba yake, kiongozi wa mbio hizo aliwataka watendaji wa halmashauri kusimamia matumizi ya fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment