21 August 2012

CWT kutetea mgomo kesho *Kuwasilisha hoja zao Mahakama Kuu *Lengo ni kuhakikisha haki inapatikana




Na Grace Ndossa

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kesho kinakusudia kukata rufaa ya kupinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Divisheni ya Kazi Dar es Salaam iliyositisha mgomo wao ambao ulikuwa ukiendelea nchi nzima.

Katika uamuzi wake Agosti 2, mwaka huu, Mahakama hiyo ilisema mgomo huo ni batili na haukuzingatia taratibu hivyo iliwataka viongozi wa CWT kuwaeleza wanachama wao warudi kazini.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Rais wa CWT, Bw.Gratian Mukoba, alisema hawakubaliani na hukumu iliyotolewa na Mahakama hiyo hivyo kesho wanakusudia kukata rufaa.

"Kesho (leo) tungeenda mahakamani kukata rufaa lakini bahati mbaya sikukuu bado inaendelea hivyo tutaenda mahakamani kesho kutwa (kesho) kukata rufaa rasmi," alisema Bw.Mukoba.

Aliongeza kuwa, tayari viongozi wa CWT wamekaa na wanasheria wao kupitia hukumu iliyotolewa na kubaini kuwa, bado wana hoja ya kukata rufaa ili waweze kupata haki yao.

Bw.Mukoba alisema hivi sasa Katibu Mkuu wa CWT, Bw. Ezekiel Oluoch, yupo mkoani Rukwa akitembelea matawi ya chama hicho na kuzungumza na wanachama.

Mahakama hiyo ilizuia kuendelea kwa mgomo wa walimu baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kubaini mgomo huo haukuwa halali hivyo iliwataka viongozi wa CWT wasitishe mgomo.

CWT imekuwa ikilaumiwa na viongozi wa Serikali kwa kukataa kukaa katika meza ya mazungumzo kama ilivyoamuliwa na mahakama.Mgomo huo ulianza Julai 30, mwaka huu.




1 comment:

  1. mpaka kieleweke bila kulipwa haki zetu hatutafanya kazi kwa moyo na kama hamuamini subiri matokeo ya wanafunzi

    ReplyDelete