21 August 2012

TASAF awamu ya tatu mwanga wa kutokomeza umaskini nchini


Na Godfrida Jola

UADILIFU katika usimamizi wa miradi ya maendeleo ni moja ya changamoto inayozikabili nchi nyingi zinazoendelea kutokana na ubadhirifu wa watendaji.

Miradi mingi imekuwa ikishindwa kutekelezwa kwa kukosa uadilifu wa wasimamizi na kuwaacha wananchi katika umaskini.

Ni viongozi wachache wanaoweza kutumia fedha zilizotengwa kukamilisha mipango iliyowekwa kutokana na tamaa ya kujilimbikizia mali.

Utekelezaji wa awamu ya pili ya TASAF ulikuwa na mafanikio makubwa kutokana watendaji wake kuwa wawazi na wenye kiu ya maendeleo kwa Taifa na kupunguza umaskini kwa wananchi.

Kutokana na uwazi miradi 11,572 imetekelezwa na kati ya hiyo, miradi  4,294  ilikuwa ya huduma za jamii, 1,405 ya ujenzi na miradi 5,875 ya makundi maalum.

Imegharamiwa na serikali kwa kushirikiana na washirika wake wa maendeleo ambapo ilitoa shilingi bilioni 32.2 na Benki ya Dunia sh.bilioni 322. Pia washirika wetu wengine walituongezea nguvu kwa kuchangia shilingi bilioni 72.

Pia, katika huduma za jamii wameboresha madarasa 5,485, ofisi za walimu 150,  nyumba za walimu 152, maabara kwenye shule za sekondari 157, majengo ya utawala katika shule za sekondari 20, mabweni ya wanafunzi 163, vyoo vya wanafunzi 705, madawati 22,946, viti 5,483, meza 4,354, vituo vya afya 63, zahanati 606, nyumba za watumishi wa zahanati 301, vyoo kwenye zahanati 339 na vituo vya maji 2,198, visima virefu 192, visima vifupi 335 na matangi ya maji 205.

Rais Jakaya Kikwete alizindua awamu ya tatu ya miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), wiki iliyopita na kusisitiza kuwa maisha bora kwa kila Mtanzania hayaji bila watu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Anasema, miradi ya ujenzi imeongezeka vijijini na kufikia 825, mabwawa madogo 78, mifumo midogo ya umwagiliaji 289, mifumo ya kuondoa maji ya mvua barabarani mita 4,593, maghala ya kuhifadhia nafaka 113, masoko 80, makaravati 901, madaraja ya watembea kwa miguu 64, na miradi ya mazingira 608 yenye walengwa 566,938.

Anasema, kwa makundi maalumu imetoa huduma kwa yatima 32,113, wajane 15,205, wazee 17,961, watu wenye ulemavu 7,840, watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI  52,316, na vijana wasio na ajira 36,859, pia watu 2,083 wamehamasishwa kujikinga na ugonjwa wa UKIMWI.

Anasema, mafanikio mengine ni vikundi 1,778 vyenye wanachama 22,712 vimeundwa kupitia Mpango wa Kuweka Akiba na Kuwekeza katika Halmashauri 44 zilizopo Tanzania Bara, Unguja na Pemba.

"Walengwa wote wamepatiwa mafunzo ya kuendesha vikundi vyao kwa ufanisi na vifaa.Mafunzo ya usimamizi, utekelezaji bora wa miradi na fani mbalimbali katika ngazi ya vijiji, wilaya na taifa yametolewa kwa walengwa 27,373," anasema.

Anasema serikali kupitia TASAF imefanikiwa pia kutekeleza Programu ya Kijamii ya Uhawilishaji Fedha kwa kaya maskini ambapo kwa majaribio katika Wilaya za Bagamoyo, Kibaha na Chamwino.

Walengwa zaidi ya 13,000 kutoka kaya 6,000 maskini na zilizo katika mazingira hatarishi zilipatiwa ruzuku ya shilingi bilioni moja na nusu kwa kujengewa uwezo ambapo watoto sasa wanapelekwa katika zahanati na vituo vya afya kwa ajili ya chanjo na kufuatiliwa maendeleo yao.


Pia watoto 1,638 ambao hawakuweza kwenda shule kwa sababu ya umaskini sasa wameandikishwa na wanakwenda shule.Kati ya wanafunzi hao, 392 wamefaulu kwenda shule za sekondari za kata.

"Wazee 4,956 wamewezeshwa kupata huduma za afya na baadhi yao wamejiunga na bima ya afya ili kupata huduma kwa urahisi na uhakika zaidi.Kutokana na mafanikio ya haraka ya programu hii, sasa maandalizi yanafanyika ili isambazwe kwenye halmashauri zote katika utekelezaji wa awamu ya tatu ya TASAF," anasema.

Anasema, changamoto katika mradi huo ilikuwa ni ya fedha kutokutosheleza mahitaji ya wananchi na uwezo mdogo wa kusimamia miradi katika ngazi mbalimbali za uongozi na uhaba wa watumishi katika vituo vya kutoa huduma ambapo uongozi wa TASAF umejipanga vizuri kukabiliana nazo

Anasema, awamu ya tatu ya TASAF itatekelezwa kwa miaka kumi, katika vipindi viwili vya miaka mitano mitano na kuweka mkazo katika miradi ya huduma za elimu, afya na maji na kuondoa umaskini wa kipato.

"Awamu hii itatoa mchango mkubwa katika kufikia malengo yetu yaliyomo kwenye  Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Mkakati wa Pili wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II) na Mkakati wa Pili wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA II)," anasema.


Anasema awamu hii inahitaji shilingi bilioni 408 ambazo zitatolewa na serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia na washirika wengine wa maendeleo.

" Serikali itatoa shilingi bilioni 45, Benki ya Dunia bilioni 330, Hispania itatoa bilioni 9, Uingereza Shillingi bilioni 24, na Marekani Shillingi bilioni 1.4. Kama ilivyokuwa kwa awamu zilizotangulia, tunawategemea sana wananchi kutuunga mkono na kuchangia kwa hali na mali," anasema.

TASAF imeonesha njia kwa miradi mingine ya maendeleo endelevu inayotakiwa kuungwa mkono na kila mtu nchini.

Viongozi wake wamekuwa wakijitoa kusimamia utekelezaji na kuhakikisha wanafanikisha walichokusudia ili kupunguza umaskini kwa wananchi.

Pia wamesaidia kutoa elimu kwa wananchi ya kusimamia miradi hiyo na kusaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.

Miradi mingi pia hukwamishwa na baadhi ya wananchi wasiopenda maendeleo hali ambayo husababishwa na kauli mbaya za watendaji kitu kilichokuwa tofauti kwa TASAF.

Ni wakati mwafaka kwa Watanzania kuiunga mkono TASAF ili kufanikisha malengo waliyojiwekea na kuondokana na dhana ya kutoondokana na umaskini.

Ushiriki mzuri na ufuatiliaji wa yanayotolewa na wawezeshaji wa miradi hiyo utamsaidia kila atakayefikiwa na mfuko huu.

Awamu ya tatu itafanikiwa zaidi ya ile ya pili kutokana na uzalendo wa viongozi wake  hivyo ni lazima ujitoa  ili kufikia lengo la maisha bora.

No comments:

Post a Comment