16 August 2012

Chanjo ya Nimonia, Kuhara kuanza Januari


Jesca Kileo na Michael Sarungi

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii, jana imezundua chanjo mbili aina ya Pneumococal na Rota Virus ya kuzuia ugonjwa wa Nimonia na Kuhara kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, ambazo zitaanza kutumika Januari 2013.

Uzinduzi huo ambao ulifanyika jijini Dar es Salaam, ulihudhuriwa na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete.

Akizungumza katika uzinduzi wa Mkutano wa Wadau wa Chanjo,  Mama Kikwete alisema mkutano huo utaleta mwamko kwa wadau na jamii iweze kuchangia na kufanikisha utekelezaji wa mkakati huo ili kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ambayo yanazuilika kwa chanjo.

Alisema imethibitika kitaalamu kuwa, chanzo hiyo ni mkakati mwafaka wa kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vya watoto.

“Hatua hii itapunguza gharama kubwa ambazo familia zetu na Taifa kwa ujumla lingetumia kutibu maradhi yatokanayo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo,” alisema Mama Kikwete.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi, alisema mkutano huo umelenga kuwajurisha wadau azma ya Serikali kuanzisha chanjo za kinga ya magonjwa hayo.

Alisema Tanzania kama nchi nyingine zinazoendelea inafanya juhudi kubwa ili kufikia malengo ya Milenia namba nne na tano ifikapo 2015.

“Takwimu za uchunguzi wa masuala ya afya za watu zinaonesha kuwa, Tanzania imeweza kupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ambao walizaliwa wakiwa hai kwa asilimia 45,”alisema Dkt. Mwinyi.

Aliongeza kuwa, viwango vya chanjo vimeendelea kupanda kutoka chini ya asilimia 50 miaka ya 1960 hadi zaidi ya 90 mwaka 2011.  

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Regina Kikuli, alisema matarajio ya mkutano huo ni washiriki kuelewa dhamira ya Serikali ya kuanzisha chanzo hizo.

Bi. Kikuli aliwataka washiriki wa mkutano kuhamasika ili kusaidia utekelezaji wa azma ya Serikali.

Alisema ni muhimu wadau na jamii kutambua umuhimu na faida ya chanjo hizo ili utekelezaji wake uweze kwenda vizuri.

No comments:

Post a Comment