16 August 2012

Balozi: Tutaimarisha ushirikiano wa kijeshi


Na Faida Muyomba

BALOZI wa Japan nchini, Bw. Masaki Okada, amesema Tanzania ni nchi yenye amani barani Afrika ambapo nchi yake itaendeleza kuipa ushirikiano wa mambo mbalimbali ya maendeleo na kijeshi.

Bw. Okada aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika hafla fupi ya kupokea meli tatu za kivita za Kikosi cha Wanamaji kutoka nchini humo ambazo ziliwasili katika Bandari ya Dar es Salaam.

Meli hizo zilikuwa na wanamaji 1,176 ambao ni Maofisa wanafunzi waliomaliza mafunzo yao nchini humo katika Chuo cha Japan Maritime Self Defence Forces (JMSDF).

“Tanzania ni nchi ya amani barani Afrika, nami nafurahia kuwepo hapa, tutaendeleza ushirikiano wetu ili kudumisha amani iliyopo kwa kuweka ulinzi thabiti,” alisema Bw. Okada.

Alisema Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kuandaa mafunzo ya pamoja kwa wanajeshi wao ili kujiimarisha zaidi katika eneo hilo ambalo ni muhimu kwa usalama wa nchi hizo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Mafunzo wa Vikosi vya Wanamaji nchini humo, Bw. Rear Admiral Hidetoshi Fuchinoue, alisema safari ya kuja Tanzania ilianza Mei 22 mwaka huu.

“Tunatarajia kuondoka Agosti 18 mwaka huu, baada ya kufanya mafunzo ya pamoja na wanajeshi wa Tanzania, hatujawahi kuja Tanzania kwa kufanya ziara kama hii hivyo tunatarajia kujifunza mengi kutokana na ushirikiano ambao tumeuanzisha,” alisema.

Kamanda wa Mafunzo na Operesheni wa Vikosi vya Majini 'Navy' nchini, Kanali Abdallah Mwemujudi, alisema mafunzo hayo yatasaidia kubadilishana uzoefu wa masuala ya kijeshi.

“Tutakuwa bega kwa bega kuendeleza uhusiano huu na kuulinda ili kuimarisha amani na utulivu wa nchi,” alisema Kanali Mwemujudi.

No comments:

Post a Comment