30 July 2012
Zanzibar kununua meli ya kisasa *Itabeba abiria 1,000, mizigo tani 100
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, ameiagiza Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, kuandaa utaratibu wa kupata fedha ndani ya wiki moja ili kununua meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,000 na mizigo tani 100.
Dkt. Shein ametoa agizo hilo jana alipofanya mazungumzoa na uongozi na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Meli ambapo kikao hicho pia kilihudhuriwa na uongozi wa Wizara hiyo pamoja na Wizara ya Miundombinu.
Katika kikao hicho maalumu Dkt. Shein alisema fedha hizo zitafutwe kutoka katika vianzio vya mapato ya ndani, nje ya nchi au kutoka taasisi ambazo zinazohusiana na mambo ya fedha.
Alisema katika kipindi kisichozidi miezi miwili, ujumbe maalumu uende kwa kampuni zinazotengeneza meli nchini Korea Kusini, China au Japan ili kutanguliza fedha kwa ajili ya meli hiyo.
Mapema uongozi wa shirika hilo, alimweleza Dkt. Shein kuwa, kaawaida ujenzi wa meli yenye ukubwa huo, huchukua mwaka mmoja hadi kukamilika.
Kikao hicho ambacho kilikuwa na lengo la kuangalia mwelekeo na mipango ya shirika hilo, kilijadili hali halisi ya meli za shirika na baadae kujadili masuala ya ununuzi wa meli mpya ambayo itaondoa usumbufu wa usafiri wa baharini kwa wananchi wanaosafiri kati ya Unguja, Pemba na Tanzania Bara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment