05 July 2012

Yanga walamba mil 20 TBL za mkutano mkuu



Na Elizabeth Mayemba

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjayo jana ilikabidhi hundi ya sh.milioni 20 kwa klabu ya Yanga kwa ajili ya kufanikisha mkutano mkuu wa klabu hiyo sambamba na uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi za viongozi waliojiuzulu.


Mkutano huo na uchaguzi wa Yanga unatarajiwa kufanyika Julai 15, mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana Kaimu Meneja wa Bia ya kilimanjaro Oscar Shelukindo alisema kiasi hicho cha fedha ni sehemu yao ya udhamini, hivyo wameona ni vyema wakakabidhi fedha hizo ili klabu hiyo ifanikishe dhumuni lake.

"Kilimanjaro Lager inatambua wajibu wake na ina nia ya dhati kuendeleza soka,kwa kuzingatia hilo tungependa kuona maendeleo ya Yanga na ndio maana tunaiunga mkono klabu hii katika mkutano wake mkuu," alisema Shelukindo.

Alisema wanatambua kuwa hiyo ni klabu kubwa yenye historia kubwa  hivyo wanaamini kuwa wanahitaji kuwa na uongozi bora, imara na madhubuti.

Shelukindo alisema wanatambua wajibu wao kama wadhamini wakuu wa klabu hiyo katika kutekeleza mkataba wao, wataendelea kushirikiana na kufanya nao kazi kwa pamoja ili kuhakikisha wanalipeleka soka la Tanzania kwenye kilele cha mafanikio.

Pia meneja huyo aliwahisi wajumbe wa mkutano mkuu kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo kwa kufanya uchaguzi wenye amani na kuchagua viongozi watakaofanya kazi kwa maslahi ya klabu.

Akipokea hundi hiyo Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesiga aliwashukuru wadhamini hao na kuwaahidi kuutumia mkutano huo kwa ajili ya kupata viongozi bora.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah alitoa rai kwa wanachama wa klabu ya Yanga kutumia mkutano mkuu kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ya klabu yao na si kuelekeza akili yao kwenye uchaguzi tu.

"Natoa rai kwa wanachama waangalie wasije wakaangalia  ajenda moja tu ya uchaguzi na kujisahau kujadili mambo mbalimbali katika klabu yao,  kwani awali uliitishwa mkutano kwa ajili ya wanachama kujua na kuhoji mambo jinsi yanavyokwenda katika klabu yao, hivyo wasijisahau na kuangalia uchaguzi tu," alisema Angetile.

No comments:

Post a Comment