05 July 2012

Mapokezi kocha mpya Yanga yafunika *Atamba fitna za kibongo anazijua


Na Zahoro Mlanzi

HATIMAYE yametimia, ndivyo unavyoweza kusema baada ya kiu ya muda mrefu ya mashabiki na wanachama wa Klabu ya Yanga, wakimsubili kocha mpya lakini jana mchana, Kocha Mbelgiji Tom Saintfeit alitua nchini kumalizana na timu hiyo.


Kocha huyo mwenye miaka 49, alipokelewa na mamia ya mashabiki kutoka sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam ambao mara baada ya kutoka nje mashabiki hao walisikika wakiimba Manji!Manji! na wengine Seif!Seif!.

Katika mahojiano yake na waandishi wa habari kwenye uwanja huo wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana, Saintfeit alisema ana furaha kupata nafasi ya kufundisha soka Tanzania.

Alisema ana uzoefu mkubwa katika kufundisha soka la Kiafrika kwani alishafanya kazi katika nchi mbalimbali zikiwemo Zimbabwe ambapo alijifunza vitu vingi kuhusu Afrika.

"Nalijua soka la Kiafrika ikiwemo Tanzania, nilipata fursa ya kuona mechi mbalimbali kupitia Supersport, hivyo sidhani kama nitapata shida," alisema kocha huyo ambaye anazungumza lugha za Kiholanzi, Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kihispania na Kiarabu.

Alisema Yanga ni timu kubwa nchini na ina mashabiki wengi ndani na nje, hivyo atajitahidi endapo wakikubaliana na viongozi wa timu hiyo kutoa ujuzi alionao.

Alisema amekuja kukamilisha mazungumzo waliyoanza na viongozi wa Yanga ambapo kama wakiafikiana baadhi ya mambo, atasaini mkataba wa kuinoa timu hiyo.

Saintfeit ametokea Nigeria nchini Nigeria ambapo alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini humo.

Kocha huyo ana leseni ya Daraja la juu la UEFA ambayo aliipata mwaka 2000, kati ya 2006 na 2007 alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Emmen FC ya Uholanzi na pia alikuwa Mshauri wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kazakhstan.

Mbali na sifa hizo, Saintfeit pia alifanya kazi kama mchambuzi wa soka katika Televisheni ya Ubelgiji na Afrika Kusini na ana elimu ya Saikolojia ya michezo.

No comments:

Post a Comment