11 July 2012

Wizara ya Ardhi yasimamisha watumishi wawili Morogoro



Na Willbroad Mathias

KATIBU Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Patrick Rutabanzibwa, amewasimamisha kazi na kuwavua madaraka Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Morogoro, Bw. Kastor Ngonyani na Msaidizi wa Kumbukumbu II, Bi. Asha Mshana kwa tuhuma za kusababisha majalada ya baraza hilo kutoka nje ya ofisi kinyume cha sheria.


Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana kwa vyombo vya habari, ilisema agizo hilo linaanza kutekelezwa mara moja ili watuhumiwa waweze kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma zinazowakabili.

Alisema katika tuhuma hizo, Bw. Ngonyani anatuhumiwa kukutwa na majalada ya mashauri yaliyofunguliwa katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nyumbani kwake wakati Bi. Mshana alisababisha majalada kutolewa nje ya ofisi za baraza kinyume cha sheria.

“Watuhumiwa wote hawataruhusiwa kuingia katika eneo la ofisi za baraza wala kutoka nje ya vituo vyao vya kazi bila ruhusa ya mwajiri wao ila wataendelea kupata mishahara yao.

“Tumelazimika kuchukua hatua baada ya Wizara kupokea taarifa mbalimbali zinazohusu migogoro inayojitokeza katika baraza hilo kutokana na ukiukwaji wa taratibu na sheria za utumishi wa umma kwa watumishi katika baraza hilo,” alisema.

Bw. Rutabanzibwa aliwataka watumishi wa Wizara hiyo kuwa makini wanapotatua migogoro mbalimbali inayohusu ardhi na kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu na sheria za utumishi.


No comments:

Post a Comment