16 July 2012

Waziri Silima aagiza watendaji kuwasaka wauza gongo nchini


Na Anneth Kagenda

JESHI la Polisi, Meya, Maofisa Tawala wameagizwa kuhakikisha wanafanya msako na kuwabaini wale wote wanaouza pombe aina ya gongo na kuwafungulia mashtaka.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Bw. Pereira Silima, wakati alipofanya ziara ya kutembelea eneo la Kigogo Mbuyuni ili kuwafariji ndugu wa waliokufa kwa kunywa pombe haramu ya gongo.


"Ninawaagiza nyie viongozi pamoja na Diwani hakikisheni watu hawa wanakamatwa na kama hamna ulinzi shirikishi basi uwepo na sisi tuko pamoja nanyi

"Mtu haruhusiwi kuuza wala kunywa pombe hii kwani ni hatari na sisi tusingependa kuwaona watu wetu wanakufa kwa kushindwa kutii sheria zilizowekwa," alisema.

Alisema kuwa tukio hilo ni la kushtua kutokana na mazingira ya watu hao kufa kwa ajili ya kinywaji ambacho Serikali ilikipiga marufuku kutokana na kwamba siyo halali.

Bw.Silima alisema pombe hiyo inawezekana ilikuwa na madhara kutokana na kwamba wanywaji wake huwa hawafi ghafla badala yake hufa taratibu taratibu kwa kuoza maini na figo.

Alisema kuwa serikali inataka wananchi wake wawe huru lakini haitovumilia kuona watu wanakufa kwa ajili ya kutumia vitu vya kuwapotezea maisha.

Alisema kuwa Manispaa ya Kinondoni  imekuwa ikituhumiwa kwa kuwa na mambo kama hayo hivyo kuwataka viongozi kuwa makini kwa kufanya misako ili kuwabaini wauaji hao.

Meya wa Kinondoni Bw. Yusuph Mwenda, alisema msiba huo umewapa majonzi makubwa kutokana na kwamba waliokufa ni nguvu kazi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Bw. Charles Kenyela, alisema kuwa wanataarifa ya kuwapo kwa mtambo wa kutengeneza gongo kati ya Kigogo na Mabobi na kusema kuwa suala hilo wanalivalia njuga na kuwataka wenye mtambo kujiandaa kukamatwa.
 
"Natangaza kihama, hatari kwa watengeneza gongo hatuwezi kuona watu wanakufa kwa ajili ya watu wachache na hivi nina vyozungumza tayari watu 12 kutoka eneo hili wamekamatwa kwa kuuza gongo," alisema.

Diwani wa Kata hiyo Bw. Richadi Chengula alisema kuwa toka matatizo hayo yameanza jumla ya watu saba wamefariki kutokana na pombe hiyo na wengine saba wako Hospitali ya Amana.

No comments:

Post a Comment