16 July 2012

Waziri Ghasia ataka wadhamini wageukie UMITASHUMTA


Na John Gagarini,Kibaha


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Hawa Ghasia ameyataka mashirika yanayodhamini michezo, kudhamini mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) ili kuboresha mashindano hayo.

Aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati akifunga mashindano hayo kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha Tumbi wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Ghasia alisema kuwa mashirika hayo yanafadhili michezo ngazi na timu zilizo madaraja ya juu na kuacha za chini ambako ndiko chimbuko la vipaji.

“Nayaomba mashirika mbalimbali yanayodhamini michezo yajiingize kudhamini na michezo hii, kwani kwa kiasi kikubwa serikali ndiyo inayodhamini mashindano haya hivyo tungeomba na wadau wengine wajitokeze kuyadhamini kwani hapa ndipo chimbuko la michezo,” alisema Ghasia.

Alisema hata hao wachezaji wanaotamba na waliotamba kwenye michezo mbalimbali miaka ya nyuma, walianzia huku kabla ya kufika huko juu walikofikia na waliko sasa hivyo lazima michezo hii isaidiwe.

“Tungependa kuona makampuni makubwa yanayozidhamini Simba na Yanga zinadhamini na hawa vijana wadogo kwani wameonesha vipaji vya hali ya juu hivyo udhamini utawasaidia kuwaongezea ari ya kucheza na kuonyesha vipaji vyao kwa umahiri zaidi,” alisema Ghasia.

Waziri Ghasia alisema kuwa michezo kama hiyo ya mashuleni inaibua vipaji ambavyo baadaye vitakuja kuikomboa nchi kwenye sekta ya michezo ndani na nje ya nchi na kuondokana na dhana kuwa Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu.

Awali akimkaribisha Waziri Ghasia Mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza alisema watahakikisha wanaboresha viwanja vinavyotumika ili wachezaji waweze kucheza kwenye viwanja vyenye ubora.

Jumla ya wanamichezo 1,517 kutoka kanda 11 walichuana kwa muda wa siku 10 kwenye michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na soka, pete, wavu, mikono, kikapu na riadha.

No comments:

Post a Comment