09 July 2012

Watalii 50,000 wajitokeza uzinduzi wa ZIFF



Na Amina Athumani, Zanzibar

WATALII zaidi ya 50,000 wamejitokeza katika uzinduzi wa tamasha la 15 la  Kimataifa la Filamu za Nchi za Majahazi ambalo hufanyika Zanzibar kila mwaka (ZIFF).

Tamasha hilo limezinduliwa juzi katika mji wa Ngome Kongwe, Zanzibar na kushirikisha wasanii, watayarishaji na waongozaji pamoja na wadau wengine kutoka nchi mbalimbali Dauniani.


Akizungumza mjini hapa wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo, Mkurugenzi Mkuu wa ZIFF,Profesa Ikaweba Bunting  aliwashukuru wadau mbalimbali  kwa kuwaunga mkono kila mwaka tangu kuanza kwa  tamasha la kwanza mpaka la sasa ambapo linatimiza kipindi cha miaka 15.

“Tunawashukuru Wazanzibar  na wageni wote kwa kuwa nasi bega kwa bega kila mwaka katika tamasha hili ambalo limekua chachu kubwa ya maendeleo na mambo mbalimbali katika msimu huu wa tamasha, hivyo tunajisikia faraja kwa kuungwa mkono” alisema Ikaweba.


Pia aliwashukuru Kampuni ya Wananchi Group, inayomiliki ving’amuzi vya ZUKU  ambao wamedhamini tamasha hilo kwa dola za kimarekani milioni moja kwa miaka 10.

Tamasha hilo lilifunguliwa na mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Ali Khalil Mirza  ambaye alilipongeza tamasha hilo kwa ukomavu wake visiwani Zanzibar na kuchangia pato kubwa la ongezeko la utalii na wageni mbalimbali wakati wa msimu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa ZIFF, Mohmoud  Thabit  Kombo aliwashukuru ZUKU kwa udhamini wao huo huku akitoa fursa na kwa kampuni nyingine kujitokeza kudhamini ilikufikia malengo zaidi ambayo yanafanywa kila mwaka na Tamasha.

Naye, Mwenyekiti wa Wananchi Group, Ali Mufuruki  alisema tamasha hilo la ZIFF lina fursa ya kipekee kwa  hapa nchini na wataendelea kushikamana bega kwa bega katika kufikia malengo ikiwemo kuendeleza sanaa  mbalimbali sambamba na kusambaza kila mahali huduma za ZUKU hapa nchini.

No comments:

Post a Comment