23 July 2012

Waokoaji Z'bar wasalimu amri *Wadai meli hiyo imezama zaidi ya mita 40 *Washindwa kuiona, waeleza ugumu wa kazi *Ofisi ya RC Dar vilio tupu, maiti zote zazikwa



Na Mwajuma Juma, Zanzibar

KAZI ya uokoaji miili ya watu waliokuwa katika meli ya Mv. Skagit iliyozama Julai 18 mwaka huu, karibu na Kisiwa cha Chumbe, Zanzibar, jana ilishindwa kuendelea baada ya meli hiyo kuzama zaidi ya mita 40 kwenda chini hivyo kusababisha wazamiaji kushindwa kuion
a.

Wazamiaji hao, jana walirudi mapema katika bandari ya Zanzibar (saa 11:30 jioni), na kuelezea ugumu wa kazi hiyo wakisubili tamko la Serikali kuhusu usitishaji wa kazi ya uopoaji miili na uokoaji.

Wakati huo huo, maiti nane kati ya 68 zilizopatikana katika meli ya Mv Skagit na kuwekwa katika viwanja vya Maisara Wilaya ya Mjini Unguja Zanzibar kwa siku tatu, zimeshindwa kutambuliwa.

Kutokana na hali hiyo, maiti hizo zimezikwa na Serikali ambapo
daktari aliyehusika na uchunguzi wa maiti, Dkt. Marijani Msafiri,
alithibitisha kuwepo maiti zilizoshindwa kutambuliwa.

Maiti hizo zimezikwa katika eneo la Kama, Wilaya ya Magharibi Unguja. Katika hatua nyingine, utambuzi wa maiti za ajali hiyo, juzi  uliingia dosari baada ya familia moja kuzika maiti mbili tofauti ambazo zote zinahofiwa si za kwao.

Familia hiyo, iliingia katika mgogoro wa kugombea maiti na baadhi ya ndugu wa marehemu Husna Ali Salum, ambaye inadaiwa alikuwemo katika meli hiyo.

Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa maiti zote ambazo walikabidhiwa familia hiyo hazikuwa za kwao.

Raia wa kikeni waliopona

Katika hatua nyingine, idadi ya raia wa kigeni kutoka nchi mbalimbali ambao waliokolewa wakiwa hai ni 14.

Juzi wageni hao walitembelewa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi walikuwemo katika ajali hiyo ya meli inayomilikiwa na Kampuni ya Seagull Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais alifika kuwajulia hali katika hoteli waliyofikia ya Serena Inn, iliyopo Shangani Zanzibar. Raia hao ni kutoka nchi za Uholanzi, Marekani, Ujerumani, Ubelgiji na mmoja kutoka Israel, alifariki ambapo hadi juzi, idadi ya abiria ambao waliokolewa ni 204.

VILIO na majonzi jana vilitawala katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, baada ya ndugu wa abiria waliosafiri na meli ya Mv Skagit, kutoona majina ya ndugu zao katika orodha ya abiria waliosafiri na meli hiyo Julai 18 mwaka huu.

Katika orodha hiyo, baadhi ya abiria wameandikwa jina moja hivyo kusababisha majina mengi kufanana ambapo wakala wa meli hiyo ambaye alizungumza na Majira kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, alisema ilibeba abiria 442 na watoto 42.

Licha ya majina hayo kujirudia, orodha hiyo (Majira inayo), ambayo imebandikwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, haionyeshi siti namba, tiketi namba, jinsi wala utaifa jambo ambalo limezua utata kwa ndugu waliofika kusoma majina hayo.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wameitupia lawama Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), kushindwa kusimamia kazi zake ipasavyo na kusababisha idadi kamili ya abiria waliopanda meli hiyo kutofahamika.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, mkazi wa Gongolamboto Bw. Majaliwa Kigosi, alisema kuwepo kwa utata wa majina hayo, kumechangiwa na wamiliki wa meli hiyo kutozingatia sheria na taratibu za usafiri wa majini.

“Tangu kutokea kwa ajali hii, sisi tumefanya kila jitihada za kumtafuta ndugu yetu Bi. Rehema au Rachel ambaye amesafiri na meli hii bila mafanikio, hata katika orodha ya wasafiri hayumo, hadi sasa hatujui la kufanya,” alisema.

Wakala mmoja wa meli hiyo (jina tunalo), amesikitishwa na orodha iliyotolewa ambayo majina mengi ya abiria hayapo.

“Mimi ni wakala kwa zaidi ya miaka 15, nasema ukweli kabisa kuwa, katika orodha hii majina mengi hayapo, mimi mwenyewe nahangaka kuwatafuta wateja zangu wawili raia wa Kenya ambao hawajaonekana hadi sasa.

“Niliwapandisha mwenyewe katika meli hii na ndugu zao kutoka Kenya wananipigia simu kila baada ya saa moja ili kufahamu kinachoendelea,” alisema wakala huyo.

Aliongeza kuwa, hadi anawapakiza wateja wake katika meli hiyo, idadi ya ilikuwa 442 na watoto 42, lakini cha kushangaza baadhi ya majina ya wateja aliowapakiza hayapo.

Hata hivyo, wakala huyo alitupa lawama kwa Jeshi la Polisi akidai limeshindwa kutumia vifaa vya ukoaji vilivyotolewa kama msaada na nchi ya Norway kabla IGP Omar Mahita, hajastaafu.

Waandishi wa wetu walifanya jitihada za kuonana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, lakini walishindwa kumpata kwa maelezo kuwa yupo nje ya ofisi.

Kutokana na hali, watu wengi waliofika kuangalia majina ya ndugu zao katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, hawajui hatma ya ndugu zao ambao wamewatafuta bila mafaniikio hadi jana.

Kutokana na utata huo, Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Meck Sadick alitoa barua kwa ndugu wasio na uwezo wa kulipia meli, kwenda Zanzibar kutafuta ndugu zao kwa meli za Kampuni ya Azam ambayo imejitolea kuwasafirisha bure ambazo zimesainiwa na Katibu Tawala mkoani humo, Bw. Edward Mbanga.

CUF yabaini uozo wa meli

Chama cha Wananchi (CUF), kimebaini uozo wa meli hiyo wakidai ndio uliosaababisha ajali kutokana na uchakavu wake.

Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema meli hiyo ilitengenezwa mwaka 1989 na kufanya kazi kwenye Washington, nchini Marekani.

Alisema mwaka 2006, meli hiyo ilisimama kubeba abiria na kuletwa Tanzania baada ya kufanyiwa matengenezo Mombasa, nchini Kenya pamoja na kuiongeza urefu.

“Inasemekani baada ya kuongezwa urefu, kumeifanya meli hii isiwe thabiti hasa kwa kubeba abiria na mizigo na ilianza kazi nchini Oktoba 2011, awali ilikuwa ikifanya safari za Unguja kwenda Pemba njini Zanzibar,baadae ilianza ruti za Dar es salaam.

“Msaada wa uokoaji ulishindikana kufanyika kwa haraka kutokana na vyombo vilivyokuwepo bandarini kukosa mafuta,” alisema Prof. Lipumba na kuongeza kuwa, uokoaji ulikuwa mgumu kutokana na hali mbaya ya hewa iliyochangiwa na upepo mkali.

Alisema waokoaji kutokuwa na taaluma yao ambao wengi wao ni watu wa kawaida, vyombo vilivyotumika katika uokoaji vilikuwa vya kienyeji hivyo havikua na uwezi mkubwa wa kuokoa.

Aliongeza kuwa, vikosi vya uokoaji vilichelewa kufika eneo la tukio ambapo chama hicho kina wasiwasi na uwezo wa manahodha pamoja na mabaharia.

Kutokana na hali hiyo, CUF wameitaka Serikali iangalie upya uwajibikaji, utendaji na mwenendo wa SUMATRA wakidai imeshindwa kuwajibika ipasavyo.

“Ni vyema Serikali ikwa na meli zake kama ilivyokuwa kwa Mv Mapinduzi na Mv Maendeleo na ziendeshwe kibiashara na faida itumike kununulia meli nyingine,” alisema.

Aliitaka Serikali kununua vyombo vya uokoaji ili yanapotokea matukio kama hayo, viweze kutumika pamoja na kutoa mafunzo ya kisasa kwa waokoaji.



SUMATRA watoa tamko

SUMATRA imesema suala la kuzama kwa meli ya Mv Skagit kwa sasa uwezi kupata mchawi mpaka Tume ikimaliza uchunguzi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano wa SUMATRA, Bw. David Mziray, alisema ni vigumu kwa sasa kubaini nani mchawi hivyo amewaomba Watanzania wasubilie tume imalize uchunguzi wake.

“Kujua nani mwenye makosa kwa sasa ni mapema mno, tusubili tume imalize uchunguzi ndipo mchawi atajulikana nani alisababisha ajali hii ambayo imeua watu wasio na hatia,” alisema Bw. Mziray.

Alisema Idara ya Hali ya Hewa, ilishatoa tahadhari na kuwataka wamiliki wa vyombo vya majini kuwa waangalifu lakini meli hiyo iliondoka bandarini Dar es Salaam kwenda Zanzibar.

Akizungumzia usajili wa meli hiyo, Bw. Mziray alisema cheti chake kilitolewa na Taasisi Umma iliyopo Zanzibar (ZMA ).

“Kwa sasa mambo mengi yataibuliwa kila mtu atasema lake bila kubaini makosa yametokea wapi, kipindi hiki tuwe watulivu na kuwafariji wenzetu waliopoteza ndugu zao,” alisema.

Aliongeza kuwa, hadi sasa mamlaka hiyo mpaka sasa imesajili kampuni 50 za meli ambazo zote zina uwezo wa kubeba tani 50 kila moja nazinafanya kazi kwa miaka 20 baada hapo hairuhusiwi kubeba abiria.

Waandishi wa habari hii ni Stella Aron, Rehema Maigala, Mwajuma JUma, Angelina Mganga, David John na Heri Shaaban.


No comments:

Post a Comment