23 July 2012
Saintief: Sasa tutalitetea kombe letu
Na Elizabeth Mayemba
BAADA ya ushindi wa juzi wa mabao 2-0 dhidi ya APR ya Rwanda Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintief amesema matumaini ya timu yake kutetea ubingwa wa Kombe la Kagame kwa sasa yameanza kuonekana.
Awali timu hiyo katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Atletico ya Burundi iliambulia kipigo cha mabao 2-0 na mechi iliyofuata wakajifariji kwa vibonde wa kundi hilo, Wau Salaam ya Sudan Kusini kwa kuichapa mabao 7-1, pamoja na ushindi huo Tom alisema bado hakuridhishwa na kiwango cha timu yake.
Akizungumza juzi mara baada ya mchezo wao na APR kumalizika, Tom alisema katika mchezo huo wachezaji wake walionesha uwezo mkubwa hali ambayo kwa upande wake ameifurahia, hivyo amewataka vijana wake waongeze bidii mchezo ujao wa robo fainali ili waweze kusonga mbele.
"Nimefurahi mno kwani APR ni timu nzuri, ambayo ipo vizuri kila idara na kila mmoja alijua tutafungwa mchezo huo lakini wachezaji wangu walifuata maelekezo niliyowapa na hatimaye wakaibuka na ushindi," alisema Tom.
Alisema awali wachezaji wake walikuwa hawajaelewana vizuri, pia aligundua kuwa hawana pumzi na ndiyo maana kila ilipokuwa ikifika kipindi cha pili walikuwa wanachoka.
Tom alisema atazidi kutoa dozi kali kwa wachezaji wake, ili kuhakikisha mechi ijayo ya robo fainali wanafanya maajabu mengine na kuzidi kuwavutia mashabiki wao kuja uwanjani kwa wingi kila timu hiyo inapocheza.
Pia kocha huyo amewataka wachezaji wake kila mmoja acheze kwa bidii, kwani hadi sasa hana kikosi kamili cha kwanza na atakuwa akiwatumia wachezaji wote ili kupima uwezo wa kila mmoja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment