31 July 2012
Wanawake Goba washauri kujiunga kwenye vikundi
Na Rose Itono
WANAWAKE waishio kwenye Kata ya Goba, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, wameshauriwa kujenga utamaduni wa kujiunga kwenye vikundi ili kujiletea maendeleo endelevu.
Wakizumgumza Majira Dar es Salaam, juzi baadhi ya wanachama wa Kikundi cha Kusaidiana cha Wanawake wa kata hiyo (KIWAKUKI), walisema umaskini kwa wanawake hauwezi kupungua kama hawatajiunga na vikundi vya kusaidiana.
Mwanachama wa kikundi hicho, Bi. Regina Maziku, alisema baadhi ya wanawake wamekuwa wakivibeza vikundi vya kusaidiana kwa sababu ya kukosa uelewa na umuhimu wake.
“Hali hii inatokana na baadhi ya wanawake kuwa na dhana tofauti kuwa, vikundi hivi vipo kwa ajili ya kupiga majungu jambo ambalo halina ukweli wowote,” alisema.
Aliongeza kuwa, ipo haja ya Serikali kutoa elimu kwa wanawake wengi zaidi hasa waishio maeneo yaliyopo nje ya mji ili waweze kuona umuhimu wa kujiunga katika vikundi hivyo.
Naye Bi. Jerumana Kikoti, alisema kuanzishwa kwa vikundi hivyo kumewasaidia wanawake kubadilishana mawazo pamoja na kuanzisha miradi ya maendeleo.
“Katika kikundi chetu cha KIWAKUKI, tuna miradi mingi ikiwemo ya upishi katika shughuli mbalimbali hivyo kutunisha mfuko wetu, pia tunakopeshana fedha mwanachama anapopata dharura na kupeana elimu ya ufugaji kuku wa kienyeji,” alisema Bi. Kikoti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment