30 July 2012
Wanamichezo kupewa ofa Quality Centre
Na Amina Athumani
WANAMICHEZO watakaofika katika maduka ya Fun Sport yaliyopo Quality Centre iliyopo barabara ya Nyerere, Dar es Salaam watapewa ofa ya kununua vitu mbalimbali kwa punguzo la asilimia 50.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Meneja Habari kwa Umma, Atuphy Mwaijengo ilieleza kwamba ofa ni maalumu kwa ajili ya mwezi huu wa mfungo wa Ramadhan.
"Quality Centre ni moja kati ya jengo lenye maduka mengi kuliko lolote hapa nchini, hivyo mbali na kutoa ofa maalumu kwenye maduka yetu ya Fun Sport pia tumeandaa michezo mbalimbali ya kuvutia kwa watoto," alisema.
Meneja huyo alisema uongozi wa Quality Centre utaendelea kuwapa watu vitu vizuri kwa ajili ya kujiburudisha katika kipindi cha mfungo wa Ramadhan.
Alisema huu ni mwanzo tu, lakini Quality Centre imepania kufanya mambo makubwa zaidi ya hayo ili kuwapa burudani na unafuu wa kununua bidhaa mbalimbali wateja wao.
"Kama tulivyosema awali maonesho ya sinema yatakuwa yakiendelea hadi saa 6 usiku, badala ya 2 kama ilivyokuwa awali na hii ni maalumu kwa ajili ya watu wanaofunga.
"Tumeona tutenge muda maalumu kwa kuwa wafungaji mara nyingi hupenda kutembea na kupunguza uchovu wa swaumu, baada ya kupata futari jioni," alisema Mwaijengo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment