03 July 2012

Wakenya watwaa ubingwa darts


Na Mwandishi Wetu

TIMU ya darts ya Triangle wanaume kutoka Kenya imetwaa ubingwa wa mchezo huo katika fainali iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Mwanza.

Mashindano hayo ambayo yalishirikisha nchi za Afrika Mashariki yalifanyika katika hoteli ya Monarch, mabingwa hao walikabidhiwa kombe pamoja na fedha taslimu sh. 200,000.


Akizungumza na wachezaji wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi, mgeni rasmi ambaye ni mwakilishi wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Flilbart Magere aliipongeza Triangle kwa kutwaa ubingwa huo na pia wachezaji wote walioshiriki mashindano hayo.

Magere alisema mchezo wa vishale sasa unapanda chati hasa Afrika Mashariki, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anauinua mchezo huo na kuutangaza, ili upate wachezaji na wapenzi wengi ambapo pia aliipongeza Tanzania kwa kuandaa mashindano hayo ambayo yalifana.

Washindi wa pili wanaume katika mashindano hayo walikuwa Lugalo ya Tanzania, ambao walipata fedha taslimu sh. 200,000 wakati wanawake nafasi ya kwanza ilichukuliwa na timu ya Nyerere ya Tanzania ambayo ilizawadiwa kombe na fedha taslimu sh. 200,000 na nafasi ya pili ni Utawala ya Kenya iliyozawadiwa sh. 200,000.

Upande wa mchezaji mmoja mmoja, nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Ibrahim Obuta kutoka Kenya ambaye alizawadiwa kombe na fedha taslimu sh. 200,000 na wa pili ni Wambura Msira wa Tanzania ambaye alipewa fedha sh. 100,000.

Kwa wanawake nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Rosemary Wanyori, kutoka Kenya ambaye alizawadiwa kombe na fedha sh. 100,000 na wa pili ni Amoding Dinah wa Uganda ambaye alizawadiwa fedha sh. 100,000.


No comments:

Post a Comment