05 July 2012

Wafanyakazi NMB Mafinga wachota milioni 80/-


Na Mercy James, Iringa

JESHI la Polisi mkoani Iringa, linawasaka watumishi wawili wa
benki ya NMB, tawi la Mafinga, wilayani Mufindi ambao wantuhumiwa kuiba sh. milioni 80.

Akizungumza na Majira jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Peter Makamba, amesema  watuhumishi hao ni Bw. Prosper Akiani na Bw. Regnard Mnuo.

Alisema uchunguzi umebaini kuwa, wizi huo ulifanyika Juni 30 mwaka huu, baada ya watuhumiwa kutoonekana kazini muda mrefu bila kutoa taarifa yoyote kwa viongozi wao.

Katika tukio jingine, mtoto Ivodia Lunyungu (2), amefariki dunia Julai 2 mwaka huu, baada ya kunywa sumu aina ya 'Thionex', akiwa nyumbani kwa wazazi wake Kijiji cha Usengeletende Kiponzelo, Wilaya ya Iringa Vijijini.

Wakati huo huo, Kamanda Makamba alisema, mkazi wa Kijiji cha Ikuku, Wilaya ya Kilolo, mkoani hapa aliyemtaja kwa jina moja la Bw. Gondwe (56), amekutwa amekufa baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kuteketea kwa moto ambao chanzo chake hakijajulikana.

Katika tukio jingine, mkazi wa Kijiji cha Kidabaga, wilayani Kilolo, Bw. Isack Ng'asakwa (22), amefariki dunia baada ya kugongwa na gari lenye namba za usajili T 293 AKL, aina ya Isuzu CVR.

Gari hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Bw. Sevelwe Kindole, ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kusababisha kifo hicho.

Alisema tukio jingine lilitokea Kijiji cha Malagosi, Wilaya ya Iringa Vijijini, ambapo mkazi wa kijiji hicho, Bi. Zuena Mgavane (24), alikutwa akiwa amekufa baada ya kujinyonga kwa kutumia shuka nyumbani kwake.

Aliongeza kuwa, Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo ambapo Bw. Kindole atafikishwa mahakaamani baada ya upelelezi kukamilika.

No comments:

Post a Comment