31 July 2012
Wafanyakazi mgodi wa Ruby wakimbia makazi
Na Mwandishi Wetu, Arusha
WAFANYAKAZI wote waliokuwa wakiishi ndani ya mgodi wa madini unaomilikiwa na Kampuni ya Mundarara Ruby Mining Company Ltd, uliopo Kijiji cha Mundarara, Wilaya ya Longido, mkoani Arusha, wameondoka mgodini hapo baada ya vijana wa kimasai (morani), kuwatangazia vita isiyo na kikomo.
Ili kuokoa maisha yao, watumishi hao waliondoka eneo hilo siku mbili baada ya Meneja wao Bw. Omari Shengovi (49), kuuawa kwa kuchomwa moto katika nyumba aliyokuwa amelala.
Watumishi hao walilazimika kutembea zaidi ya kilomita 30 kwa miguu hadi Kijiji cha Kitumbeine kabla ya kutumiwa usafiri na Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw. Philip Mkenga 'Jungle Master'.
Habari zilizopatikana ambazo zilithibitishwa na viongozi wa Serikali wilayani humo, zimedai Morani hao wakiwa katika mkutano wa hadhara na viongozi wa Serikali, akiwemo Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. James Millya, ghafla walitangaza kuvamia mgodi huo.
Morani hao walidai kuwa, kitu chochote ambacho watakikuta ndani ya mgodi huo kitakuwa halali yao ambapo kutokana na vitisho hivyo, viongozi wa kimila na Serikali akiwemo Mbunge wa jimbo hilo, Bw. Lekule Laizer, walituliza fujo hizo bila mafanikio.
Inaelezwa kuwa, kutokana na hali hiyo viongozi wa kimila na Serikali walilazimika kuwaomba watumishi hao kuondoka eneo la mgodi mara moja ili kuepusha maafa mengine na kulita Jeshi la Polisi liingilie kati ili kulinda usalama wa mgodi.
Akizungumza na Majira jana kwa njia ya simu, Ofisa Taarafa ya Longodo, Bw. Peter Kakanyi, alisema hali si shwari katika eneo hilo kwani morani hao bado wana hasira ya kuuawa kwa mwenzao, Momeli Ole Ingeremunu (28), ambaye alipigwa risasi baada ya kuingia ndani ya mgodi huo akiwa na wenzake
“Ni kweli watumishi wa mgodi huu wamelazimika kuondoka na kutembea umbari mrefu kwa miguu ili kunusuru maisha yao baada ya morani kutishia kufanya mauaji mengine katika mgodini wao.
“Mkutano kati ya morani, viongozi wa kimila na Serikali ulivunjika lakini jitihada zinaendelea ili kutafuta suluhu,” alisema Bw. Kakanyi.
Kwa upande wake, Bw. Millya ambaye alizungumza na Majira kwa njia ya simu, alithibitisha kutokea kwa hali hiyo na kukiri ugumu uliopo katika kutafuta muafaka wa suala hilo lakini juhudi zinaendelea.
“Wakati tukiendelea na mkutano wa kutafuta suluhu, ghafla morani wakatangaza vita upya na watumishi wa mgodi, tulijitahidi kutuliza hasira zao bila mafanikio hivyo tukalazimika kuepusha maafa kwa kuwataka watumishi wa mgodi waondoke mara moja, hivi sasa mgodi unalindwa na askari wa Jeshi la Polisi,” alisema Bw. Millya.
Aliongeza kuwa, leo wataendelea na vikao vya kutafuta suluhu ya mgogoro uliopo ili kurejesha amani iliyopotea kati ya pande hizo kwani tayari jamii hiyo imekubali kurudisha mahusiano.
Hata hivyo, baadhi ya watumishi wa kampuni huyo hasa walinzi na wadhibiti madini katika mgodi huo ambao walizungumza na gazeti hili walisema hawapo tayari kurudi katika mgodi huo kwani maisha kwao yana thamani kubwa kuliko madini.
“Maisha kwetu ndio mtaji, hatuwezi kukubali kuyapoteza kirahisi kwa kupambana na watu wasioelewa thamani ya maisha, hatupo tayari kurudi tena mgodini,” alisema mlinzi wa mgodi huo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Usiku wa kuamkia Julai 25 mwaka huu, inadaiwa zaidi ya morani 500 walivamia mgodi huo na kumuua Meneja wa kampuni hiyo kwa kuichoma moto nyumba aliyokuwa akiishi wakati akiwa ndani.
Morani hao pia wanadaiwa kuchoma moto gari la kampuni hiyo, mashine ya upepo mgodini na kuharibu mali mbalimbali ambazo zinakadiriwa kuwa thamani ya zaidi ya sh. milioni 300.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment