04 July 2012

Wafanyakazi 679 wapandishwa vyeo



Na Eliasa Ally, Iringa

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa imewapandisha vyeo wafanyakazi 679 kutoka katika idara mbalimbali kutokana na wao kuonesha juhudi za utendaji kazi mzuri.

Wafanyakazi waliopandishwa vyeo wamehimizwa kufanya kazi kwa moyo na kuendeleza jitihada za kuleta maendeleo katika sekta zao wanazozihudumia.


Akizungumza jana na Majira ofisini kwake Ofisa Utumishi kwa Umma wa Halmashauri ya Mufindi Bw. Lameck Machino alisema kuwa wafanyakazi hao wamepandishwa vyeo kulingana na muundo wa utumishi wa kila kada na kuwaongezea ari ya uwajibikaji.

"Tumewapandisha vyeo kwa kuzingatia vigezo vya nafasi zao, uwepo wa fedha katika bajeti ya serikali, ubora wa kiutendaji katika sekta zao, kujituma pamoja na wale ambao wanajiendeleza kitaaluma tunawapandisha vyeo," alisema Bw. Lameck Machino.

Alisema kuwa, Halmashauri ya Mufindi inatilia maanani kuhusiana na kuwapandisha vyeo watumishi ambao wanakidhi vigezo na sifa walizonazo ambapo aliongeza kuwa hali hiyo itawatia moyo wafanyakazi na kuhamasika zaidi katika shughuli zao wanazozifanya kila siku serikalini.

Alizitaja baadhi ya idara ambazo wafanyakazi wake wamepandishwa vyeo katika mwaka wa 2012/2013 kuwa ni Elimu ya Msingi wafanyakazi 364, Elimu ya Sekondari 126, Utawala 22, Afya 62, Maendeleo ya ya Jamii 11 ambapo wafanyakazi wengine waliopandishwa wanatoka katika idara za fedha, mipango, ujenzi, kilimo na ushirika pamoja na ardhi maliasili na mazingira.





No comments:

Post a Comment