04 July 2012
Chatanda ajitosa kuwalipia leseni waendesha pikipiki
Na Yusuph Mussa, Korogwe
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Bi. Mary Chatanda ametangaza kulipa gharama za leseni kwa baadhi ya madereva wa bodaboda na bajaji mjini Korogwe baada ya kubaini vijana wengi hawana leseni hizo.
Pamoja na kuwalipia vijana hao zaidi ya 350 leseni zenye thamani ya sh. milioni 18.5 pia amewataka kuanzisha chama chao na kwa kutambua kuwa vijana wengi wameajiriwa kuendesha bodaboda hizo, atakiweza chama hicho kuwa na pikipiki zake kama mradi.
Alitoa ahadi hizo juzi kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa madereva wote wa bodaboda mjini Korogwe yanayofanyikia mjini hapa huku yakiendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la APEC kutoka Dar es Salaam na Jeshi la Polisi.
"Mafunzo haya ni muhimu kwa vijana wetu kuondokana na ajali za mara kwa mara, hivyo kwa kufahamu mchango wa bodaboda ambao umetoa ajira kwa vijana wengi, hivyo naahidi kulipia leseni kwa vijana wote ambao wamehudhuria mafunzo haya.
"Lakini pia nawataka muunde chama chenu ambacho kitajadili kero mbalimbali mnazopata. Na ni rahisi pia kwenda kumuona OCD kupitia umoja wenu, najua wengi mmeajiriwa, lakini chama chenu nitakiwezesha kuwa na pikipiki zake ili uwe mradi wenu," alisema Bi. Chatanda.
Bi. Chatanda alimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa APEC Bw. Respicius Timanywa fedha taslimu sh. milioni moja ili aweze kununua projekta yenye thamani ya sh. milioni 1.3 inayoonesha mafunzo kwa matukio ukutani.
Hata hivyo Bw. Timanywa alisema ni viongozi wachache wenye moyo wa kutoa kama alivyo Bi. Chatanda, kwani tangu ameanza kutoa mafunzo jijini Dar es Salaam na sasa wanakwenda mikoani, hawajawahi kupata msaada wa namna hiyo.
"Bi. Chatanda ameonesha moyo wa kuisaidia jamii, kwani kuwalipia hawa vijana leseni ambayo kila mmoja inagharimu sh. 53,000 ili kuikamilisha ni msaada mkubwa. Hata sisi tunashukuru kwa kupata projekta, itatuwezesha kutoa mafunzo vizuri," alisema Bw. Timanywa.
Mgeni rasmi katika mafunzo hayo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Korogwe Bw. Madaraka Majiga alisema wamegundua bodaboda ni jeshi kubwa kama watalitumia vizuri vitendo vya uhalifu vitapungua nchini, kwani wao watakuwa sehemu ya Polisi Jamii.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
SIDHANI KUNA WILAYA YENYE BODABODA WENGI MKOA WA TANGA KAMA KOROGWE VIJANA NI WENGI WILAYANI KOROGWE SIDHANI WANAPATA UWAKILISHI MZURI KWA MBUNGE ALIYEPO IDADI KUBWA YA VIJANA WALIOJITOKEZA MBUNGE ALIYEPO AJIPANGE VIZURI
ReplyDelete