04 July 2012

Halmashauri zatakiwa kuwajibika kikamilifu



Na Salma Mrisho, Geita

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Bi. Hawa Ghasia amezitaka halmashauri zifanye kazi zake kwa umakini na uadilifu ili kuepusha lawama na mianya ya rushwa hali inayopelekea kwenda kinyume na taratibu za kazi.


Hayo aliyasema jana, alipokuwa akizungumza na madiwani, wakuu wa idara na watumishi wa serikali mkoani Geita akiwa katika ziara ya kuhamasisha utendaji bora wa kazi na usimamizi wa mamlaka za serikali za mtaa na kuwakumbusha wajibu wao.

Alisema kuwa, ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) inaonesha kuwa wilaya zote za mkoani Geita zimepata hati zenye mashaka na Wilaya ya Geita imepata hati hiyo miaka miwili mfululizo na kuongeza kuwa mara nyingi hati zenye mashaka kuna uwezekano wa kutumbukia kwenye hati chafu.

Alisema, ikiwa halmashauri imepata hati chafu maana yake itanyimwa ruzuku ambayo pia inawaathiri wananchi ambao waliwachagua madiwani kuja kusimamia halmashauri hususan mapato na matumizi wapange kwa niaba yao.

Bi. Ghasia aliongeza kuwa wapo madiwani ambao ni wajumbe wa Kamati ya Fedha ambao wanawawakilisha wenzao ambapo huwa wanaambiwa zimeingia shilingi ngapi, zimetumika kiasi gani na wana wajibu wa kwenda kukagua miradi ya maendeleo na kuona imetekelezwa kwenye kiwango sahihi ikiwemo kuhoji kama haijatekelezwa ipasavyo.

“Sasa kama hamkufanya hayo yote mpaka akaja mkaguzi na kusema anawapa hati chafu, ipo haja ya halmashauri ikanyimwa pesa ili madiwani wapate hasira na wasimamie kazi ipasavyo na upo ushahidi, hata kitabu cha CAG mwaka huu kimewataja baadhi kwa majina jamani msiache mambo yaende bila kujua undani wake matokeo yake ndiyo haya mnayaona wenyewe,”alisema Waziri  huyo.

No comments:

Post a Comment