18 July 2012
Wafanyabiashara wa madini walia na bei leseni ya ununuzi dhahabu
Na Said Njuki, aliyekuwa Shinyanga
WAFANYABIASHARA wa madini ya dhahabu mikoa ya Tabora na Shinyanga, wameiomba Serikali kuangalia upya malipo ya leseni za ununuzi wa madini hayo ambayo hivi sasa imefikia sh. milioni moja badala ya sh. 250,000.
Ombi hilo limetolewa juzi mjini Shinyanga kwa viongozi wa Chama cha Wanunuzi na Wauzaji Madini nchini (TAMIDA) na kudai kuwa, ongezeko hilo ni kikwazo ambacho kinawafanya washindwe kumudu gharama za malipo hayo.
“Sisi mitaji yetu ni kidogo hivyo ongezeko hili inachangia kuua familia zetu, tunaiomba Serikali itupunguzie kwa sababu Serikali yetu ni sikivu,” alisema Bw. Joseph Temela.
Mwenyekiti wa TAMIDA nchini, Bw. Sammy Mollel, alisema wataangalia jinsi ya kutoa mapendekezo kwa Serikali ili kuimarisha na kukuza biashara hiyo kwa wazawa na kuongeza thamani ya uuzwaji wake nje ya nchi.
Bw. Mollel ambaye yupo katika ziara maalumu kwenye mikoa ya Kanda mbalimbali nchini alisema lengo la kuanzishwa kwa chama hicho ni kuwaunganisha wafanyabiashara na Serikali ili waweze kufanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni ya madini hayo.
Aliwaongoza wafanyabiashara hao mkoani Shinyanga kufungua tawi la TAMIDA, kufanya uchaguzi ambapo Bw. Joseph Temela, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na Bw. Gregory Kibusi, kuwa Katibu wakati Bw. Majid Ahmed (Mweka Hazina).
Wengine waliochaguliwa ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao ni Bw. Ayub Aboubakari na Bw. Ally Yena. Bw. Temela aliahidi kufanya kazi kwa uwazi na kuwatumikia wanachama kwa adilifu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment