18 July 2012
Polisi wanaokataa Rushwa sasa kuzawadiwa
Na Benedict Kaguo, Dodoma
SERIKALI imeanzisha utaratibu mpya wa kutoa zawadi kwa askari polisi ambao wataonesha uwajibikaji wa kukataa kupokea rushwa wanapotekeleza majukumu yao.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emanuel Nchimbi, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/13.
Alisema Jeshi la Polisi limeendelea kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya watendaji wake ambao wanajihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.
Aliongeza kuwa, mwaka wa fedha 2011/12, malalamiko 625 ya wananchi dhidi ya kero za rushwa kwa polisi yalishughulikiwa ambapo askari 68 walifukuzwa kazi huku na wengine 9 kesi zao zinaendelea katika mahakama za jinai.
“Askari wengine 15, uchunguzi wa kesi zao bado unaendelea kutokana na makosa ya rushwa, Serikali pia imeongeza posho ya chakula kwa askari kutoka sh.100,000 kwa mwezi hadi sh. 150,000 ili kuongeza morali ya kazi na kupunguza ukali wa maisha.
“Kiwango hiki ambacho ni kipya pia kitatumika kwa Jeshi la Magereza, Zimamoto na Uokoaji pamoja na Idara ya Uhamiaji,” alisema Dkt. Nchimbi.
Aliongeza kuwa, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuboresha masilahi ya askari ambazo ni pamoja na kuanza kutumika kwa kanuni za fidia kwa askari ambao wanaumia au kuuaawa wakiwa kazini ambapo mwaka wa fedha 2011/12, askari 62 waliumia na 16 kuuawa.
Alisema askari hao au wategemezi wao, wanastahili kulipwa fidia kati ya sh. milioni moja na sh. milioni 15 kwa walioumia na wategemezi wao kulipwa sh. milioni 15 kwa askari ambaye ameuawa akiwa kazini.
Dkt. Nchimbi alisema mwaka wa fedha wa 2012/13, Jeshi la Polisi linatarajia kuajiri askari wapya 3,000 ambapo idadi kubwa ya waajiriwa itapatikana kutoka shuleni na Vyuo vya Elimu ya Juu.
“Utaratibu huu umelenga kuwa na askari wenye sifa stahiki na waaminifu katika kazi hii, suala la Uhamiaji mwaka wa fedha 2011/12, Watanzania 34 walipata uraia wa mataifa mengine.
“Mataifa hayo ni Namibia, Uingereza, Ujerumani, Norway, Kenya, Botswana, Denmark, Korea ya Kusini, Marekani, Afrika Kusini na Cuba hivyo kupoteza haki ya kuwa raia wa Tanzania kwa mujibu wa sheria ya uraia namba 6 ya mwaka 1995,” alisema.
Alisema kipindi cha Julai 2011 hadi April 2012, wageni 14,781 walipewa hati za ukaazi nchini ukilinganisha na wageni 12,563 waliopewa hati hizo kipindi kama hicho mwaka 2011.
“Idadi ya hati zilizotolewa imeongezeka na kufikia 2,218 sawa na asilimia 17.7, hali hii ni matokeo ya kuanza kuimarika kwa uchumi duniani na hatua zinazochukuliwa na Serikali za kuboresha
mazingira ya uwekezaji,” alisema Dkt. Nchimbi.
Akizungumzia urai, Dkt. Nchimbi alisema wageni 18 walipatiwa uraia ambao wanatoka nchi za India, Kenya, Pakistani, Somalia na wawili kutoka Pakistani ambao ni wanawake wameolewa na Watanzania na kutoka Somalia, watoto saba raia wa nchi hiyo tayari ni raia wa Tanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment