06 July 2012

Wadau kuifufua Tukuyu Stars upya



Na Janath Abdulrahimu

WADAU na wapenzi walioguswa na kupotea kwa timu ya Tukuyu Stars ya Mbeya, wameanzisha mkakati wa kuifufua na kuirejesha Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza Dar es salaam jana Mratibu wa mpango huo, Kennedy Mwaisabula alisema ili kufikia malengo yaliyowekwa na wadau mbalimbali wameanza utekelezaji wa mchakato huo ukihusisha wadau wa Dar es Salaam na waliopo mkoani Mbeya.


"Tumeguswa na tuna uchungu mkubwa kuona Tukuyu Stars haipo tena katika ramani ya soka, hivyo tumekusudia kuirejesha tena tukianzia kusaka vipaji vijijini mkoani Mbeya," alisema Mwaisabula.

Alisema ili kuleta hamasa na kuibua vipaji vitakavyounda, Tukuyu Stars Family imeanzishwa ligi ndogo wilayani Rungwe ili kusaka wachezaji ambapo ligi hiyo itamalizika Agosti 4, mwaka huu.

Mwaisabula alisema  siku ya fainali ya ligi hiyo kutakuwa na mechi za vijana chini ya umri wa miaka 14 na 17 zikihusisha timu waalikwa watakaoshindana na wenyeji, ngoma za asili, ikifuatiwa na mechi ya wakongwe waliowahi kuicheza Tukuyu Stars miaka hiyo ambapo maveterani wa Dar es Salaam, watachuana na wale wa Mbeya.

Alisema kilele cha shughuli hizo itahitimishwa rasmi na kongamano la kuifufua Tukuyu stars.
Pia kutakuwa na mjadala utakaohusisha kuiendesha timu kama kampuni, uuzaji wa hisa za kampuni na upatikanaji wa bodi na watendaji wa timu.

No comments:

Post a Comment