10 July 2012
Wadau: Bajeti ya kutangaza utalii iongezwe
Na Mwandishi Wetu
WADAU wa utalii katika sekta binafsi nchini, wameiomba Serikali kuongeza bajeti ya utangazaji utalii kwa Bodi ya Utalii nchini (TTB) ili iweze kumudu ushindani na kutangaza vivutio vya Tanzania katika nchi mbalimbali duniani.
Walisema bajeti injayotengwa kwa TTB ni ndogo ambayo haikidhi shughuli nzima ya utangazaji vivutio husika pamoja na kuipongeza bodi hiyo kwa ushirikiano mkubwa wanaotoa kwa wadau ili kuitangaza nchi katika sekta ya utalii.
Wadau hao waliyasema hayo Dar es Salaam mwishoni mwa wiki walipokutana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki katika chakula cha jioni.
“TTB inafanya juhudi kubwa za kutangaza vivutio mbalimbali vilivyopo ndani na nje ya nchi lakini bajeti ambayo wanapewa na Serikali kufanikisha jukumu hili ni ndogo sana,” walisema.
Waliongeza kuwa, mbali ya watendaji wa bodi hiyo kuwa nao katika maonesho na misafara mbalimbali ya utangazaji utalii duniani ambayo wanaitaribu, pia wanashirikiana kuandaa mikakati ya kuitangaza nchi.
“Tunashukuru hivi sasa kwa kushirikiana na TTB, tuko katika mchakato wa kukamilisha mpango mkakati wa kuitangaza Tanzania” alisema Katibu Mtendaji wa TCT Bw. Richard Rugimbana.
Katika hafla hiyo, Balozi Kagasheki alisikiliza matatizo mbalimbali yanayowakabili wadau hao na kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto hizo.
Aliitaka TTB kubuni mbinu za kujiingizia fedha badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini ambayo haitoshelezi na kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa ili kuboresha maendeleo ya sekta hiyo.
“Wizara yangu itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kutokana na mchango wenu mkubwa katika sekta hii, ninyi ndio watu mnaotoa huduma kwa watalii katika nyanja mbambali.
“Mchango wenu ni mkubwa sana katika maendeleo ya utalii nchini, nawaahidi kuwa Wizara yangu itaendelea kutoa ushikiano kwenu,” alisema Balozi Kagasheki.
Hii ni mara ya kwanza Balozi Kagasheki kukutana na wadau hao tangu ateuliwe kuiongoza Wizara hiyo na kutaka kuwepo mikutano ya namna hiyo mara kwa mara ili kubadilisha mawazo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment