17 July 2012
Vinara wa vurugu kupinga bei ya pamba wakamatwa
Na Suleiman Abeid, Shinyanga
JESHI la Polisi mkoani Simiyu, linawashikilia watu tisa wanaodhaniwa kuwa vinara wa vurugu zilizotokea hivi karibuni wilayani humo zilizofanywa na wakulima wa zao la pamba wakipinga bei ya sh. 660 kwa kilo moja.
Akizungumza na Majira, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Salum Msangi, alisema jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watu hao kutokana na kundi lililoibuka ambalo linachochea vurugu, kuchoma moto maghala ya kuhifadhia zao hilo na kuharibu magari ya kampuni za ununuzi wa pamba.
Alisema chanzo cha vurugu ni wakulima kupinga bei iliyotangazwa na Serikali sh. 660 kwa kilo, kuzuia wanunuzi kwenda kununua pamba vijijini kwa bei hiyo na kuwataka wakulima wengine kutouza zao hilo kwa bie hiyo.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Bw. Ndembi Mboje (42), Bw. Ndila Puga (19), Bw. Mishamu Tenwa (59) na Bw. Tengo Manyangu (67) wote wakazi wa Kijiji cha Bunamhala.
Wengine ni Bw. Mbugani Theophil (56), mkazi wa Kijiji cha Ngh’wamwita, Bw. Charles James (31), wote wakazi wa Kibara Bunda, mkoani Mara na Bw. Masanja Sita, mkazi wa Kijiji cha Luguru.
“Katika vurugu hizi ambazo zilitokea Kijiji cha Bunamahla, wakulima waliteketeza kwa moto nyumba moja ya mkazi wa kijiji hiki ambayo ilikodiwa na Kampuni ya NGS Co. Ltd, kwa ajili ya kuhifadhia pamba.
“Pamba yote ambayo ilikuwa ndani ya nyumba hii nayo iliteketea kwa moto, pia waliharibu gari aina ya Scania lenye namba za usajili T. 551 AVN, ambalo lilivunjwa vunjwa vioo kwa mawe,” alisema.
Hata hivyo, Kamanda Msangi alisema polisi walifika eneo la tukio kabla ya kutokea madhara makubwa na kutumia nguvu ya ziada kuutawanya umati wa watu waliokuwa eneo hilo.
Aliongeza kuwa, vurugu nyingine zilitokea juzi usiku kwenye Kijiji cha Bukingwaminzi ambapo baadhi ya wakulima wasiotaka bei hiyo, walizingira gari jingine la Kampuni ya NGS na kutaka kulichoma moto wakidai lilitaka kusafirisha pamba.
“Polisi walipofika eneo hilo, walilazimika kutumia mabomu ya mchozi na silaha za moto hewami ili kuwatawanya wananchi ambao tayari walikuwa wamelizingira gari lililokuwa likipakia pamba.
“Gari hili lilikwenda katika jijiji hicho kusomba pamba ambayo ilinunuliwa kutoka kwa baadhi ya wakulima waliokubali kuuza zao hili kwa bei ya Serikali ili kuipeleka kiwandani,” alisema.
Alisema pamoja na polisi kuwatawanya wananchi, tayari gari hilo lilikuwa limeharibiwa vibaya kwa kuvunjwa vioo, taa zake za mbele na nyuma ambapo watuhumiwa watafikishwa mahakamani hivi karibuni baada ya uchunguzi kukamilika.
Wakati huo huo, Mbunge wa Maswa Magharibi, Bw. John Shibuda
amemuomba Rais Jakaya Kikwete, kutoa kauli juu ya mtafaruku wa bei ya pamba ambao umesababisha vurugu kwa wakulima wa zao hilo katika Wilaya za Bariadi, Maswa na Meatu, mkoani Simiyu.
Bw. Shibuda alitoa ombi hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari kutokana na vurugu zilizosababisha baadhi ya watu wamejeruhiwa, nyumba mbili kuchomwa moto na uharibifu wa magari ambayo yalivunjwa vioo na taaa.
Alisema Rais Kikwete anapaswa kutoa tamko kuhusu bei ya zao hilo sh. 660 kwa kilo moja ambayo imepingwa na wakulima kwa
madai hairejeshi gharama walizotumia katika kilimo hicho.
Aliongeza kuwa, Serikali haitoe kipaumbele kwa zao hilo hivyo mkulima amekuwa akitangatanga bila kujua la kufanya kutokana na bei ya pamba kuyumbayumba kila mwaka na kuwachosha wakulima ambao hivi sasa wameaanza kujichukulia sheria mkononi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment