17 July 2012
Uwekezaji miundombinu chachu ya maendeleo sekta ya utalii
Na Suleiman Abeid
HALMASHAURI ya wilaya ya Meatu mkoani Simiyu ni moja ya halmashauri nchini inayomiliki maeneo ya hifadhi ya wanyamapori kandokando na Hifadhi za Taifa za Serengeti, Ngorongoro na Maswa Game Reserve.
Baadhi ya halmashauri za wilaya zimekuwa zikishindwa kunufaika na mapato yanayotokana na utalii katika maeneo yao kutokana na aidha kutokujua njia sahihi za kuyaendesha maeneo hayo kwa njia za kibiashara au kwa kukosa utaalamu wa jinsi ya kuingia ubia na wawekezaji katika sekta hiyo.
Kutokuwepo na mipango endelevu ya kuendeleza maeneo ya hifadhi sehemu hiyo imekuwa ikikumbwa na uharibifu wa mazingira kunakosababishwa na baadhi ya wananchi kuendesha shughuli za kibinadamu ikiwemo ukataji miti hovyo na uchomaji wa mkaa.
Mbali ya uharibifu huo, pia kumekuwepo na makundi ya wawindaji haramu wa wanyama mbalimbali bila vibali hali ambayo husababisha halmashauri husika kupoteza mapato kutokana na wanyama wanaowindwa katika hifadhi zake.
Hata hivyo serikali kwa upande wake imekuwa ikitoa elimu ya mara kwa mara juu ya umuhimu wa utunzaji wa hifadhi za wanyamapori na kuihamasisha jamii juu ya suala zima la utunzaji wa mazingira katika maeneo yao.
Pia imeweza kuwashirikisha wananchi wa vijiji 525 katika wilaya 63 nchini ili waweze kushiriki katika kusimamia misitu 37 ya hifadhi ya serikali kuu pia Halmashauri za wilaya yenye jumla ya hekta 1,863,623.
Miongoni mwa Halmashauri zenye maeneo hayo ya hifadhi ni pamoja na wilaya ya Meatu mkoani Shinyanga, ambayo kwa upande wake inafanya kila juhudi ili kuhakikisha hifadhi hizo zinawaingizia kipato wakazi wa wilaya hiyo tofauti na siku za nyuma.
Juhudi hizo ni pamoja na kuanza harakati za kuingia ubia na baadhi ya wawekezaji wanaojishughulisha na shughuli za kitalii ikiwemo uhifadhi wa mazingira, wanyamapori na utalii wa upigaji picha.
Utaratibu huu utasaidia kuipatia mapato Halmashauri hiyo kwa kila mwaka hii ni pamoja na serikali za vijiji vilivyoko katika eneo la hifadhi (WMA) ambapo watakuwa wakipata asilimia kidogo katika pato litakalolipwa na wawekezaji.
Wilaya hiyo inamiliki eneo la hifadhi ya wanyamapori linalopakana na hifadhi ya Serengeti na ya Maswa Game reserve ambapo vijiji saba vinavyozunguka eneo hilo viliungana na kuanzisha Hifadhi ya Jamii ya wanyamapori (WMA).
Katika kuhakikisha hifadhi hiyo inawanufaisha wakazi wa Meatu, uongozi wa halmashauri hiyo kupitia Baraza la madiwani wameingia makubaliano na mwekezaji mzawa Kampuni ya Mwiba Holding Limited yenye makao makuu yake mkoani Arusha ili iwekeze katika hifadhi hiyo ya WMA.
Kampuni ya Mwiba iliyopewa eneo lenye ukubwa wa hekta 19,600 katika kijiji cha Makao imefunga mkataba na halmashauri ya Meatu ambapo ambapo katika mkataba wa awali mwekezaji huyo atakuwa akiilipa halmashauri hiyo kiasi cha shilingi milioni 100 kwa mwaka.
Shughuli zitakazoendeshwa na kampuni hiyo katika eneo ililokabidhiwa kuwekeza ni pamoja na zile za utalii wa upigaji picha, uwindaji na ufugaji wa wanyama ambao watalii mbalimbali wa ndani na nje ya nchi watakuwa wakienda kuwaangalia.
Mbali ya malipo hayo kampuni hiyo pia itasaidia miradi mbalimbali ya maendeleo na ile ya kijamii ikijikita zaidi katika suala zima la elimu ambapo imetoa mchango mkubwa katika kuanzisha shule ya sekondari katika kijiji cha Makao ambayo itatumiwa na watoto wa jamii ya wafugaji.
Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Mwiba, Bw. Nyaga Mawala, anasema mbali ya kuilipa halmashauri ya wilaya ya Meatu kiasi hicho cha shilingi milioni 100 kwa mwaka, lakini pia kampuni yake itajikita zaidi katika kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii wilayani humo.
“Mbali ya malipo tunayopaswa kulipa kila mwaka, lakini pia kampuni itatoa sehemu ya mapato yake kusaidia mambo ya elimu, hili liwe ni sharti mojawapo katika uwekezaji wetu na pia tutahakikisha panaanzishwa mfuko wa elimu na mfuko wa dhamana ili kuweza kuwahakikishia kipato cha kudumu wanakijiji cha Makao,” anasema Bw. Mawala.
Bw. Mawala anasema eneo hilo la ufugaji wanyama litakalojulikana kama ranchi ya wanyamapori ambalo ni ya aina yake nchini litakuwa na itakuwa ni mfano wa kuigwa katika uanzishwaji wa ranchi nyingine katika maeneo mengine ambako ardhi yake imekaa bila kutumika kikamilifu kuingiza mapato kwa wakazi wake.
Anasema kampuni yake hivi sasa inafanya utaratibu wa kuisaidia halmashauri ya wilaya ya Meatu katika kuanzisha kikosi maalumu cha ulinzi ili kuimarisha ulinzi katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori (WMA) iliyoko katika kijiji cha Makao.
Anasema katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na matukio mabaya yanayofanywa na baadhi ya majangili wanaovamia eneo hilo hali ambayo inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kusababisha watalii kuogopa kutembelea hifadhi hiyo.
“Matukio ya ujangili katika eneo la hifadhi yanachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi ya watalii, ninaishauri halmashauri yetu iangalie uwezekano wa kuunda kikosi maalumu kwa ajili ya ulinzi katika eneo lote la WMA na kule katika kijiji cha Makao,”
“Binafsi kampuni yetu ipo tayari kutoa wataalamu ili kuweza kufundisha vijana wa Meatu juu ya taaluma ya uendeshaji wa masuala ya ulinzi katika maeneo ya hifadhi za wanyapori, ninachoomba tushirikiane katika kuboresha ulinzi katika eneo hilo ,” anasema Bw. Mawala.
Anasema hivi sasa kampuni yake imekamilisha ujenzi wa viwanja viwili vya ndege ambapo kimoja kimejengwa katika eneo la hifadhi kijiji cha Makao na kingine katika eneo la Bulyanaga nje kidogo ya mji wa Mwanhuzi.
Bw. Nyaga anasema kukamilika kwa ujenzi wa viwanja hivyo kutarahisisha mawasiliano ya haraka kwa watalii watakaokuwa wakitembelea eneo hilo tofauti na walipokuwa wakilazimika kutumia uwanja wa ndege ulioko katika mkoa wa Arusha.
Anasema mbali ya uwanja uliopo katika kijiji cha Bulyanaga kilometa 15 kutoka mjini Mwanhuzi kutumiwa na ndege za kampuni yake lakini pia uwanja huo utatumiwa na wasafirishaji wengine wa kampuni za ndege zinazosafirisha abiria kutokana kuwa na uwezo wa kutua ndege zinazobeba abiria 25.
Kwa upande wake mshauri mwelekezi wa Kampuni ya Mwiba, Bw. Joseph Masina anasema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa viwanja hivyo viwili katika hatua za awali ambapo hivi sasa ndege zinatua na kuruka pasipo tatizo, kampuni yake imeanza hatua ya pili kwa kujenga miundombinu muhimu.
Bw. Masina anasema moja ya vipaumbele ni ujenzi wa nyumba za watumishi, jengo la abiria la kusubiria usafiri pamoja na vifaa vya mawasiliano ikiwemo rada ya kuongozea ndege katika uwanja uliopo katika kijiji cha Bulyanaga.
Anasema pia tunatarajia kuuimarisha uwanja huo kwa kuweka molamu katika njia ya kutua na kurukia ndege pamoja na kuifanyia ukarabati mkubwa barabara inayotoka mjini Mwanhuzi mpaka uwanjani ili kurahisisha usafiri wa abiria watakaokuwa wakiutumia uwanja huu.
“Hivi sasa tumeishakabidhiwa rasmi eneo la ardhi lenye ukubwa wa ekari 20 baada ya kumalizika kwa mgogoro mkubwa kati ya halmashauri ya wilaya na wanakijiji waliokuwa wakimiliki eneo hilo ambapo kampuni kwa niaba ya uongozi wa halmashauri imelipa kiasi cha shilingi 8,450,000 kwa wamiliki hao,” anasema Bw. Masina.
Anasema uwepo wa uwanja huo utasaidia kwa kiasi kikubwa ongezeko la kipato kwa wakazi wa wilaya ya Meatu kutokana na wasafiri pamoja na watalii wengi watakaopitia hapo kuweza kufanya biashara mbalimbali na wakazi wa Meatu ikiwemo nyumba za kulala wageni na hoteli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment