27 July 2012

Uturuki sasa kumaliza kero ya mgawo



Na Stella Aron

MGAWO wa umeme nchini, unaweza kusahaulika na kubaki historia baada ya wajumbe wa kampuni kubwa 16 kutoka nchini Uturuki ambazo zinahusika na uzalishaji nishati hiyo, kuwasili nchini ili kubadilishana mawazo na sekta nyingine.


Hayo yamebainika Dar es Salaam jana katika mkutano ambao ulishirikisha wafanyabiashara mbalimbali nchini na wajumbe wa kampuni hizo ambazo zinahusika kuzalisha umeme nchini humo.

Akizunguma na wajumbe hao, Balozi wa Uturuki nchini Bw. Ali Davutoglu, alisema Tanzania ina uwezo mzuri kibiashara na uchumi kama itapata wawekezaji wakubwa na kuifanya iweze kufikia malengo yake kiuchumi.

Alisema kuwa endapo wafanyabiashara wa Tanzania watakutana na ujumbe huo wenye uzoefu kibiashara na kubadilishana mawazo namna ya kuboresha sekta ya nishati na sekta zingine ana imani kuwa tatizo linaloisumbua nchi la umeme linaweza kupungua kama si kumalizika kabuisa.

Alisema Tanzania ina soko kubwa lenye biashara kama itapata fursa na usimamizi nzuri hivyo siku tatu ambazo wajumbe hao watakua nchini na kufanya ziara kwenye kampuni mbalimbali zikiwemo zinazozalisha nishati nchini, tatizo la mgawo linaweza kukoma.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Mhandisi Aloys Mwamanga, alisema kuwa wafanyabiashara wengi nchini wana fursa ya kushirikiana na ujumbe huo, kubadilishana mawazo na kufikia makubaliano mazuri ili kuinua uchumi na kuchochea maendeleo.

Kwa upande wake, Mfanyabiashara kutoka Kampuni ya Pipeline and Tanskl Inspector Bw. Toto Golan, alisema kama Tanzania ikiamua kuwekeza katika masuala ya nishati ya upepo na jua, upo uwezekano wa tatizo la mgawo wa umeme kupungua au kwisha kabisa.

Alisema nchini Uturuki hakuna tatizo la mgawo ambapo kwa asilimia kubwa, vifaa vya umeme vinavyouza nchi za Ulaya vinatoka nchini humo.

Ujumbe huo unatarajiwa kutembelea ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO Ubungo), Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Mauzo ya Nje (EPZA), Ofisi za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Temeke na Shirika la Simu Tanzania (TTCL).

No comments:

Post a Comment