23 July 2012

Utoro wa wabunge wakwamisha bajeti *Ni ya Wizara ya Kilimo, CCM watupiwa lawama *Hoja yaibuliwa na Mbatia, tamko zito latolewa



Na Benedict Kaguo, Dodoma

BUNGE jana lilishinda kupitisha bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kutokana na idadi ndogo ya wabunge waliokuwa ndani ya ukumbi huo.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Spika Bw. Job Ndugai, alilazimika kulihairisha kutokana na matakwa ya kanuni za Bunge zinazotaka kuwepo nusu ya wabunge ili uamuzi uweze kufanyika.

Hatua hiyo imekuja siku chake baada ya Bi. Makinda kuwaonya wabunge kuwa, tabia ya utoro iliyojengeka ipo siku Bunge litashindwa kupitisha bajeti jambo ambalo limetokea jana.

Baada ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza kuhitimisha majibu ya hoja za wabunge na kuingia katika Kamati ya Matumizi ya Bunge ili kupitia vifugu, Mbunge wa kuteuliwa Bw. James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisimama na kuomba mwongozo wa Spika.

Bw. Mbatia alisema, kwa mujibu wa katiba na kanuni ya 77 ya Bunge, imeeleza wazi kuwa hayatafanyika maamuzi yoyote hadi kuwepo nusu ya wabunge ndani ya ukumbi huo hivyo alimuomba Spika kuhairisha Bunge kwani maamuzi yawawezi kufanyika kwa mujibu wa kanuni hiyo.

Alisema idadi ya wabunge wote ni 352 lakini wabunge waliokuwemo ndani hazidi 110, ambapo nusu ya wabunge wote ni 176 hivyo kuendelea kupitisha bajeti hiyo ni kuvunja kanuni.

Hatua hiyo ilibua mjadala ambapo Bw. Ndugai alieleza vipengele vya vifungu viendelee kupitishwa hadi mwisho wa kuhitimisha ndipo atatoa mwongozo wake kama idadi ya wabunge waliokuwemo inakidhi kufanya maamuzi.

Baada ya wabunge kumaliza kupitia vifungu hivyo, Bw. Ndugai alijiridhisha kuwa idadi ya wabunge haikutosheleza hivyo kulazimika kuhairisha Bunge hadi kesho.

“Wabunge wengi wamekwenda Zanzibar kuwafariji wafiwa na waathirika wa ajali ya meli ya Mv. Skagit,” alisema Bw Ndugai.

NCCR-MAGEUZI wakutana na waandishi

Baada ya bunge kuhairishwa, Bw. Mbatia na wabunge wa chama hicho akiwemo Bw. Felix Mkosamali (Muhambwe), Bw. Moses Machali (Kasulu Mjini), Bw. David Kafulila (Kigoma Kusini) na Bi. Agripina Buyogera (Kasulu Vijijini), ambapo walitoa tamko la chama hicho.

Bw. Kafulila alisema chama hicho kitamwandikia barua Spika wa Bunge Bi. Anne Makinda, kumtaka atoe orodha ya wabunge wote tangu mkutano wa bunge la bajeti uliopoanza Juni 12 mwaka huu na kama itathibitika kuwa orodha haikutimia wakati wa kupitisha bajeti zilizopita, itabidi maamuzi hayo yabatilishwe kwani ni batili.

Alisema kwa muda mrefu chama hicho kimeshuhudia kuwepo idadi ndogo ya wabunge lakini maamuzi yamekuwa yakifanyika mara kwa mara hivyo orodha hiyo itabaini ukweli na lazima maamuzi yote yaliyofikiwa yatenguliwe.

Kwa upande wake, Bw. Machali alisema utoro wa wabunge unachangiwa na udhaifu wa Kanuni za Bunge zinazosema mbunge ataondolewa kuwa mbunge kama hatahudhuria mikutano mitatu mfululizo jambo ambalo linachangia udhaifu huo.

“Kanuni hizi ni dhaifu sana, mbunge ataondolewa ubunge kama hajahudhuria mikutano mitatu maana yake Bunge lote la bajeti tangu Juni hadi Agosti lipite likiwemo la Novemba na Februari ndio anaondolewa sifa ya kuwa mbunge ndio maana utoro unaota mizizi” alisema Bw. Machali.

Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Maswa Mashariki Bw. John Shibuda (CHADEMA), alisema bajeti hiyo imekwamishwa na wabunge wa CCM ambao ndio wengi.

Alisema wabunge wa CCM wanafanyakazi kwa matakwa yao si ya wananchi waliowatuma kuwatumikia ambapo mahudhurio kidogo ni ishara kuwa na utengano kati ya Bunge na Serikali ya CCM.

“Mahudhurio madogo ni ujumbe tosha kuwa hawakubaliani na utekelezaji wa ilani ya CCM, umoja na mshikamano wa wabunge wa CCM ni hafifu ndio maana hawahudhurii vikao,” alisema.


Alikosoa mtindo wa kupitisha bajeti bila kupata muda mrefu wa kuijadili akidai ni sawa na kufunika maovu ambayo yangejadiliwa kwa kina bungeni.

No comments:

Post a Comment