23 July 2012

Makinda ampa pole Dkt. Shein



Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Bi. Anne Makinda, amemtembelea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, ili kumpa mkono wa pole kutokana na ajali ya kuzama kwa meli ya Mv. Skagit.

Bi. Makinda ambaye alikwenda Ikulu ya Zanzibar pamoja na baadhi ya wabunge wa Bunge la Muungano, alisema viongozi na Watanzania wameguswa na ajali hiyo pamoja na kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na viongozi wa Serikali zote.

Kwa upande wake, Dkt. Shein alitoa shukerani za pekee kwa Bunge la Muungano na ujumbe wake kwa niaba ya wabunge, kuueleza ujumbe huo jinsi tukio hilo lilivyotokea na juhudi zilizofanywa na Serikali zote kupitia vyombo yake vya ulinzi, usalama pamoja na wananchi walivyoshiriki katika uokoaji.

Alitumia fursa hiyo kuvipongeza vikosi hivyo, wananchi na wamiliki wa vyombo vya baharini kwa kushiriki kikamilifu katika suala zima la uokoaji na kuongeza kuwa hadi jana, watu ambao wameokolewa walikuwa 145 na maiti 68.

“Miongoni mwa waliookolewa ni pamoja na watalii 14, mmoja alifariki dunia, Serikali zote mbili zinaangalia namna bora zaidi ya kujiandaa na uokoaji katika ajali kama hizo pamoja na kujenga uwezo zaidi katika matukio kama haya,” alisema.

Aliongeza kuwa, juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha kasoro zilizokuwepo, zinapunguzwa au kuondolewa kabisa ukiwemo uhaba wa vifaa na utaalamu katika uokoaji.

Dkt. Shein alisema waokoaji wamefanya kazi kubwa na kuongeza kufika kwa viongozi hao ni kutokana na mapenzi waliyonayo kwa pande mbili za Muungano.

Wakati huo huo, salamu za rambi rambi zimeendelea kutolewa kwa Dkt. Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepokea taaarifa za tukio hilo kwa masikitiko makubwa, majonzi na huzuni.

Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), umetoa mkono wa pole na kuunga mkono uokoaji uliofanyika baada ya ajali. Salamu nyingine za pole zimetolewa na ubalozi wa Vietnam nchini, India na Misri.

Bodi ya Wakurugenzi na Wanachama wa Jumuiya ya Kampuni zinazotembeza watalii Zanzibar (ZATO), nao wametoa mkono wa pole na kueleza jinsi walivyopokea tukio hilo kwa mshtuko.

No comments:

Post a Comment