06 July 2012

Utafiti: Mazingira ya biashara Tanzania bado magumu



Na Hyasinta Timothy

WAWEKEZAJI na wafanyabiashara Tanzania wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinatokana na mazingira ya biashara kuwa magumu na kushindwa kujiendesha kwa faida.

Ripoti ya nne ya kila mwaka ya mitazamo ya viongozi wa biashara nchini inatoa muhtasari wa mawazo yao juu ya mazingira wezeshi na nafasi ya serikali katika kuhakikisha biashara zinafanywa kwa urahisi.

Ripoti hiyo imeandaliwa ili kutoa vidokezo juu ya masuala ya vipaumbele vya kufanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.

Utafiti wa maoni ya wadau wa biashara juu ya mazingira ya uwekezaji Tanzania uliofanyika 2011 ulibainisha maoni ya wadau wa biashara kuhusu mazingira ya uwekezaji.

Kazi ya kukusanya taarifa za utafiti zilifanywa na Synovate kati ya Juni na Julai, 2011. Majibu yao yalifanyiwa uchambuzi na ripoti iliandikwa na mchambuzi na mtaalam wa masuala ya uchumi, Bw.David Irwin. 

Ripoti hiyo iliratibiwa na BEST-AC taasisi ambayo kazi yake ni kuzisaidia taasisi za sekta binafsi (PSOs) kujihusisha katika mazungumzo kati ya sekta binafsi na ya umma kwa lengo la kushawishi mabadiliko katika sera za umma zenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara Tanzania.

Utafiti huo unaonyesha kuwa mambo yanayoongoza katika kuweka ugumu katika kuendesha biashara na kuzifanya zisikue kama inavyotakiwa ni pamoja na umeme, barabara, rushwa na maji.

Umeme umekuwa ni tatizo la mara kwa mara na barabara zikishika nafasi ya pili. Rushwa, ambayo ilionekana kupungua mwaka 2010, imerudi tena na kuwa ni tatizo kubwa

Maji ambayo hayakutajwa kuwa ni tatizo hadi mwaka 2010, sasa yanaonekana kuwa katika hali mbaya, ugumu wa upatikanaji wa fedha (mitaji) umeshuka kidogo, ingawa watunga sera wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kwa sababu bado ni tatizo katika uboreshaji wa mazingira ya biashara.

Benki ya Dunia inaeleza kuwa uboreshaji wa mazingira wezeshi ya biashara utasaidia kuongeza kiasi cha uwekezaji kwenye sekta binafsi, hali itakayosaidia kuwanufaisha wawekezaji na wafanyabiashara na ajira itaongezeka na kupunguza umaskini.

Njia nzuri kwa serikali kuelewa mbinu za kutumia kuboresha mazingira wezeshi ya biashara ni kuwa na mazungumzo na mashauriano na sekta binafsi na hasa kutambua na kushughulikia mahitaji ya sekta hiyo katika mambo ya vipaumbele.

Bw.Irwin anasema matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa mitazamo ya viongozi wa biashara haijabadilika sana kati ya mwaka 2009 na 2011, hali inayoakisi pia tathmini ya Benki ya Dunia juu ya utafiti wake wa ufanyaji biashara.

Anasema Benki ya Dunia hufanya tafiti mbalimbali kuangalia masuala mbalimbali kisha huyachapisha matokeo kwenye ripoti ya kila mwaka inayojulikana kama 'Doing Business'.

Anasema ripoti hiyo inatoa mwongozo na kipaumbele cha mazingira ya biashara. Nchi nyingi zimekuwa zikichukua hatua kutokana na matokeo ya ripoti hiyo kwa lengo la kupunguza urasimu na kuleta mabadiliko.

Bw. Irwin anasema ripoti ya mitazamo ya viongozi wa biashara Tanzania iliangalia kama masuala ambayo yamo ndani ya uwezo wa serikali yanapewa kipaumbele chochote katika kushughulikia masuala yanayoleta mazingira mazuri ya biashara.

Vitu ambavyo kwa wastani vilionekana kuboreka ni mawasiliano ya simu usalama, sheria ya ajira, sheria ya mazingira, nguvukazi yenye ustadi, mikataba ya kisheria, urahisi wa kusajili ardhi, bandari na viwanja vya ndege, leseni na kanuni.

Sera za uchumi mkubwa, usimamizi wa kodi, upatikanaji wa mitaji, kiasi cha kodi, barabara, maji, rushwa, umeme.

Bw.Irwin anasema masuala ambayo serikali inatakiwa kuyapa kipaumbele kulingana na umuhimu wake ni nishati na rushwa kwani vinaonesha vinaendelea kuongezeka kwa kasi ikilinganishwa na vitu vingine.

"Maji yana kipaumbele zaidi. Barabara imebakia kuwa muhimu na hivyo kuonesha jinsi vipaumbele vilivyobadilika tangu mwaka 2008," anasema.

Ripoti ya Benki ya Dunia ya 'Doing Business' 2012, inaiweka Tanzania kwenye nafasi ya 127, nafasi ambayo haitofautiani na mwaka jana. Nafasi yake katika maeneo muhimu ya kufanya biashara nayo imebaki palepale.

Anasema inaleta maana zaidi kama tutalinganisha jitihada za Tanzania na nchi nyingine kwenye ukanda huu. Rwanda ilishika nafasi ya kwanza kwa mwaka 2009 kulinganisha na ripoti ya Doing Business ya mwaka 2010, ambapo ilipanda kwa nafasi 76, na kwa mwaka 2010 ilishika nafasi ya pili katika kuleta mabadiliko, ambapo ilipanda kwa nafasi 9.

"Kwani mwaka 2011 nafasi ilirekebishwa kwenye Doing Business ripotiya 2012, kwa hiyo Tanzania ikaporomoka kutoka nafasi ya 125 hadi kushika nafasi ya 127,"anasema.

Ripoti za Benki ya dunia zina faida zaidi kwa watunga sera katika kutoa mwanga kwenye maeneo yanayohitaji kufanyiwa mabadiliko.

Pia ripoti hizo zinasaidia kuwasukuma watu wengi kuanzisha biashara au kujihusisha kwenye uchumi wa sekta binafsi unaotegemea zaidi juu ya maoni mengi juu ya urahisi wa kufanya biashara kuliko kutegemea ripoti inayatoa maoni ya ujumla yaliyotolewa katika 'Doing Business'.

Anasema maoni yatasidia kwa asilimia kubwa na si yatawashawishi watunga sera kwamba kuna mambo zaidi wanatakiwa kuyafanyia kazi, bali pia pale kwenye tofauti kuwa kati ya maoni ya hali halisi, itaisaidia serikali vidokezo jinsi ya kuwasiliana na wahusika kujua hali halisi.

Anasema ripoti hiyo inatenganisha masuala ambayo ni muhimu kwa kila sekta, kwani kuna masuala mengi ambayo kwa umoja yanasaidia kuleta mazingira wezeshi kwenye biashara, ni muhimu kwa kila biashara, na siyo vyote vinasababisha ugumu katika kufanya biashara.

"Utafiti huu umefanyika si tu kwa vipengelee vinavyoleta matatizo, bali pia tofauti na tafiti nyingine inawauliza viongozi wa biashara kuainisha vipengele ambavyo serikali inaonekana kufanya kazi nzuri," anasema.

Anasema ripoti hiyo ilijaribu kukusanya gharama wanazopata kwa ajili ya mahitaji ya kisheria yanayowekwa kwenye biashara.

Ripoti hii ya nne inaonesha kuwa maeneo ya vipaumbele yamebadilika kidogo, hasa inajidhihirisha kwenye vipaumbele vilivyoainishwa mwaka jana.

Anasema gharama za sheria linatakiwa kuwa eneo la kipaumbele kwa serikali yetu kuchukua hatua kama inataka kuleta mabadiliko na si tu katika mazingira wezeshi bali jinsi inavyochukuliwa na watu wanaofanya biashara.

"Tanzania kwa sasa imekuwa ikifanya jitihada kubwa ili kubadili nafasi yake kwenye ripoti ya Doing Business na imekuwa ikitafuta mawazo na taarifa kutoka sekta binafsi, "anasema.

Serikali na sekta binafsi wanaonekana kushirikiana kwa pamoja na kufanya mazungumzo katika kuandaa sera na kukubaliana katika kuleta mabadiliko ya kisera, ambayo yatasaidia kuboresha mazingira ya kufanya biashara, na mwishowe kuwa na uwekezaji zaidi, ajira na mapato zaidi ya kodi.

Utamaduni uliojengeka katika wizara mbalimbali umeanza kubadilika, ingawa hakuna nafasi ya kuleta mabadiliko kwa asilimia kubwa.

Hatua hiyo inatoa changamoto kwa sekta binafsi  kuitumia vizuri nafasi hii ya uwazi kwenye serikali.

Mchambuzi wa ripoti hiyo Bw.David Irwin, anasema idadi ya watu walioshiriki katika utafiti huo ilikuwa ni biashara 157 ikihusisha sekta na maeneo mbalimbali na hata ukubwa tofauti.

Anasema katika ripoti hiyo umeme au mawasiliano ya simu yanaweza kuwa yanapatikana kwa uhakika. Masuala mengi yameonekana mengi yanaonekana kwa ni muhimu.

Anasema suala la rushwa lilionekana si muhimu ukilinganisha na masuala mengine ambayo yameonekana ni muhimu kwa asilimia 75 kwa waliojibu dodoso hizo.

Anasema masuala manne yaani umeme, barabara, mawasiliano na usalama yanaonekana kama muhimu kwa asilimia 95 kwa maoni wadau wa biashara.

Pia rushwa ilishika nafasi ya chini kwa umuhimu wake labda kama biashara hiyo inategemea rushwa ili ifanikiwe lakini inaweza kuingilia kwenye ufanisi wa utawala na mafanikio ya biashara.

Anasema umuhimu wa masuala yanayofanya uendeshaji biashara kuwa mgumu ni usalama, nguvu kazi yenye ujuzi, urahisi wa kusajili ardhi upatikanaji fedha, mazingira, leseni na kanuni sera za uchumi mkubwa, rushwa, mawasiliano ya simu, bandari na viwanja vya ndege barabara, maji na umeme

Masuala yanayofanya ufanyaji biashara kuwa magumu ni moja ya masuala yaliyododoswa na majibu yalikuwa katika usalama, nguvu kazi yenye ujuzi urahisi wa kusajili ardhi, upatikanaji fedha, mazingira, leseni na sera za uchumi mkubwa rushwa, mawasiliano ya simu, bandari na viwanja vya ndege, barabara, maji na umeme.

Pia umuhimu wa masuala ambayo hayatakiwi kukatiwa kodi yameshuka tangu tangu mwaka 2010, ubora na vyeti vya kuuza nje vituo vya mizani barabarani, utaratibu wa uhamiaji
mfumo wa forodha.

Ingawa vikwazo vyote vya msuala yote matano vinachukuliwa na wafanyabiashara wachache kuwa vinachangia kufanya biashara kuwa ngumu, kwa wahojiwa wengi wanaona kuwa siyo tatizo hata kidogo.

Vikwazo visivyo vya kodi vinavyoleta ugumu kwenye biashara ni ubora na vyeti vya kuuza nje, vituo vya mizani barabarani, utaratibu wa uhamiaji, mfumo wa forodha.

Hata hivyo ni muhimu kukumbuka kuwa, wakati vikwazo visivyo vya kodi vinaweza kuwa ni tatizo kwa idadi ndogo ya biashara, vinaweza kuwa ni tatizo kubwa kwa biashara hizo na kuleta madhara makubwa.

Kwa mfano vikwazo vinavyozuia muunganisho wa bara au vinaongeza urasimu kusafirisha bidhaa nje vinaweza kusababisha ucheleweshaji kwa wenye viwanda na wasindikaji lakini wanaweza wasilichukue kwenye tathmini yao ya mazingira.

Mwaka 2010 mawasiliano ya simu yalionekana kuwa na matokeo mazuri. Kwa vipengele vingi kulikuwa na mitizamo kuwa serikali ilikuwa ikifanya jitihada kidogo katika kuboresha mazingira wezeshi ya biashara.

Anasema kuwepo kwa mfumo mmoja wa kufanya haya yote bado ingeiwezesha serikali kupata mapato kutoka kwenye sekta hii huku ikiweka mfumo madhubuti ambao unapunguza gharama ya kufanya biashara na kuwapatia muda wafanyakazi kwa kujihusisha na kazi za kutafuta masoko, kutoa mafunzo na kujenga mahusiano na wateja.

Wafanyabiashara wengi wangekuwa tayari kulipa kodi kama zingewekwa kwenye mkondo mmoja na kuwepo kwa uwazi jinsi fedha hizo zinavyotumika.



No comments:

Post a Comment