05 July 2012

Utafiti kilimo cha chai kuwanufaisha wakulima Mufindi


Na Eliasa Ally

UTAFITI wa kilimo cha chai unaofanywa na watafiti mbalimbali kutoka kwa Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania wanasaidiwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) ambayo inawasaidia katika wilaya ya Mufindi mkoani Iringa ni suluhisho kwa kuwainua wakulima.


Pia, itawaendeleza zaidi kiuchumi hali ambayo inaleta muafaka wa kunufaika zaidi kwa wananchi kutokana na sekta ya kilimo.

Watafiti hao ambao tayari wamewasaidia elimu wakulima katika kutambua na kukabiliana na changamoto mbalimbali wamekamilisha utafiti wao, ambapo pia wanasema kuwa zao la  chai endapo litalimwa, litahudumiwa na kuuzwa katika soko kiusahihi litawakomboa wananchi, litaingiza kipato serikalini na nchi kwa ujumla itanufaika.

Kabla ya utafiti huo wa kilimo cha zao la chai, wakulima wengi katika wilaya hiyo walikata tamaa kutokana na kupata hasara baada ya kuuza chai kwa bei ndogo.

Mtafiti wa zao la Chai katika wilaya ya Mufindi Prof Bruno Ndunguru akizungumzia hali halisi ya kilimo cha chai walibaini udongo kukosa rutuba mbadala kwa zao la chai, ambapo wakulima hao waliingia makosa zaidi kwa kutumia mbolea kupanda na kuyakuzia swala ambalo lilipelekea kuharibika kwa ardhi na hatimaye kukosa kabisa rutuba kwa zao la chai.

Prof. Ndunguru anasema hatua za kwanza     EU ilisaidia kujenga majengo mapya ya ofisi ambazo zitatumika kwa watafiti wa kilimo hicho kwa wakulima wadogo wadogo wa Mufindi, ambapo walitoa milioni 500 zilizotumika kujenga majengo, vifaa vya kufanyia utafiti hadi kufikia mafanikio sahihi.

Prof. Ndunguru anasema, " Utafiti wetu ulihusisha zao la chai kwa kutafuta aina mpya ya mbegu na miche ya kupandwa, uwezo wa kusambaza maji katika mashamba ya chai, rutuba sahihi ya ardhi na kujenga ofisi za kutosha kwa ajili ya kazi nzima ya utafiti,".

Anaongeza kuwa katika kufanya kazi ya kutafiti udongo na ardhi sahihi kwa kilimo cha chai wamehakikisha aina zote unapimwa katika maabara zao za kilimo katika ofisi zilizojengwa wilayani Mufindi, kutoa ushauri sahihi wa matumizi sahihi ya ardhi kwa kulima chai, kutoa taarifa za maeneo ambayo wakulima walitumia mbolea za chumvi pamoja na kuhamasisha masoko yanayonunua chai.

Anasema kuwa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya imesaidia fedha hizo 500 katika hatua za kukamilisha mikakati hiyo ili kuwezesha zao la chai kuwa na faida zaidi kwa wakulima wenyewe, kuliingizia taifa mapato makubwa yenye tija na kuwahamasisha wananchi wengine ambao hawajaanza bado walime chai.

"Misaada ambayo imetolewa na Jumuiya ya Ulaya kwa awamu tofauti ambapo awamu ya kwanza ya mwaka 2001 hadi 2004 EU walitoa pesa kusaidia na awamu ya pili ya mwaka 2005 hadi 2008 kuwa zilitolewa pesa zingine na kukamilisha milioni 500 kuendeleza mradi huu", anafafanua Prof Ndunguru.

Anasema katika hatua nyingine balozi wa EU Bw.Filberto Gerian Sebregand ameongeza pesa nyingine sh milioni 300 kwa ajili ya kuendelea kupanua wigo wa utafiti, kilimo, masoko na kuboresha usafirisha baada ya kufurahishwa na hatua zilizofanywa na watafiti hao na matumizi sahihi ya pesa za awamu ya kwanza.

Prof Ndunguru anasema katika mwaka wa 2001 hadi 2004 mradi uliwahusisha wakulima wa chai wa wilaya ya Mufindi 4,350,364, ambapo katika mwaka wa 2005 hadi 2008 wakulima walikuwa 13,987,901 na kuanzia mwaka 2009 hadi 2012 jumla ya wakulima 24,828,387 hali ambayo inahamasisha EU waendelee kutoa misaada zaidi ya pesa kuwakomboa wakulima hawa.

"Mradi huu wa kilimo cha chai unalenga zaidi kupata mazao yanayotokana na chai yaliyo katika ubora wa viwango sahihi, kuongeza uzalishaji, idadi ya wakulima na ubora wa chai yenyewe, kutumia teknolojia ya kisasa zaidi ya katika kukabiliana na changamoto za masoko pamoja na changamoto za usafirishaji, usindikaji na masoko ya wanunuzi wa chai duniani", alifafanua Prof Bruno Ndunguru.

Mwenyekiti wa kamati ya Utafiti Dkt. Emmanuel Simbua anasema kuwa wakulima watanufaika moja kwa moja katika kulima zao la chai kwa kusomesha watoto, kujenga nyumba za kisasa, kuhimili hali ya kiuchumi kwa kupata kipato kikubwa tofauti na hapo awali ambapo wakulima walikuwa wamekata tamaa.

Dkt. Simbua anaongeza kuwa zao la chai lipo kati ya mimea ambayo ni tiba kwa baadhi ya magonjwa yanayomkuta binadamu kwa nyakati tofauti ambapo kwa kunywa chai ya rangi inayotumia majani ya chai kila wakati kwa mtu anaweza kupona magonjwa yakiwemo ya kansa, moyo, kuondoa kisukari na afya ya binadamu kuimarika wakati wote.

Dkt. Simbua anasema kuwa Mamlaka ya Utafiti wa Chai ya Taifa TSRAT imefanya utafiti ambapo kati ya hekta 47,416 ni za misitu ya asili ekari ambapo 7,123,000 zinalimwa chai na wakulima wadogo wadogo na kuwa misitu ya kupandwa ili kuimarisha zao la chai ni hekta 16,690 na kufikisha jumla ya hekta za misitu kuwa 64,106 na hekta zinazolimwa chai kuwa 80,000 zinalimwa na kampuni za chai.

"Ardhi ni rasilimali kubwa sana katika nchi yoyote ambayo ukiitumia vizuri katika shughuli za kiuchumi, kwa sasa katika wilaya ya Mufindi sekta ya kilimo imeweza kuajiri watu kwa asilimia 70 ambapo uchumi katika wilaya ya Mufindi kutokana na zao la chai umekua kwa asilimia 85 unaokwenda moja kwa moja kwa wananchi, hii ni hatua kubwa kiuchumi", anasisitiza Dkt. Simbua.

Baadhi ya wakulima wa chai wa wilaya ya Mufindi Bw, Emmanuel Lugano, Jackson Mwampulule, Labson Mahenge na Ibrahim Sanga anasema, kutokana na kulima kilimo cha kisasa baada ya watafiti kufanya utafiti wa chai sasa wanaweza kuwa na uhakika wa maisha ikiwemo kusomesha watoto na kuboresha maisha yao.

"Awali sisi wakulima tulikata tamaa kabisa kuendelea kulima chai, utafiti uliofanywa na watafiti hawa, umetukomboa kutokana na sasa tunalima kilimo bora, tunapata soko la uhakika na tunaweza kuhimili changamoto mbalimbali za kiuchumi tofauti kabisa na hapo awali tukipata hasara",.




No comments:

Post a Comment