05 July 2012

TFF yataka Watanzania kuwa wazalendo



Na Shufaa Lyimo

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah amewataka Watanzania kuonesha uzalendo kwa timu za Tanzania zitakapokuwa zinacheza na timu za nje katika michuano ya Kombe la Kagame itakayoanza kutimua vumbi Julai 14,mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam juzi Osiah alisema uzalendo ni kitu muhimu katika mashindano hayo kutokana kuwa ni njia tosha ya kuwapa morali wachezaji wa hapa nchini.

Katibu huyo alikemea tabia ya baadhi ya mashabiki, ambao wamekuwa wakizizomea timu za Tanzania wakati moja wapo inapokuwa imefanya vibaya na kushangilia timu pinzani, hali ambayo haioneshi picha nzuri.

"Naomba Watanzania tuzisapoti timu zetu wakati zitakapokuwa zinacheza, pamoja na kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwashangilia vijana wetu," alisema.

Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa  Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholous Musonye amesema maandalizi kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Kagame, yamekamilika na kuzitaka timu shiriki kusikiliza makocha wao.

Alisema wachezaji wanatakiwa kuonesha viwango vya hali ya juu kutokana na kuwa mashindano hayo yatawasaidia kujulikana nje ya nchi na kupata nafasi ya kwenda nje kufanya majaribio kupitia kwa mawakala watakaokuwa hapa nchini.

"Kagame ni mashindano makubwa muhimu, ambayo yatawatangaza wachezaji wetu pia ni wakati wa wao kujitangaza wenyewe," alisema Musonye.

Timu zitakazoshiriki mashindano hayo  ni Yanga, Azam FC na Simba (Tanzania), APR (Rwanda), URA (Uganda), Wau Salaam (Sudan Kusini), Mafunzo (Zanzibar), Vita (Burundi), Ports, (Djibouti) na Tusker (Kenya)

No comments:

Post a Comment