04 July 2012

Ufisadi wa trilioni 11.6/-



Na Benedict Kaguo, Dodoma

MBUNGE wa Kisesa, mkoani Simiyu, Bw. Luhaga Mpina (CCM), amefichua ufisadi wa sh. trilioni 11.6 ambazo Taifa linapoteza kutokana na watumishi wa Serikali na wafanyabiashara kuficha fedha za umma nje ya nchi bila kuchunguzwa.


Alisema katika taarifa ya The global Financial Integrity (GFI) ya mwaka 2008, inaonesha Tanzania kwa miaka 39 kuanzia 1977 ni nchi ya 13 kati ya 20 zinazoongoza kwa utoroshaji wa fedha za umma na kuzificha nje.

Aliongeza kuwa, tangu kipindi hicho hadi sasa, Tanzania imepoteza sh. trilioni 11.6 ambazo zimefichwa nje na wafanyabiashara pamoja  na watendaji wa Serikali.

Bw. Mpina alisema licha ya taarifa za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na Serikali za Mitaa kuonesha ufisadi wa fedha za umma kutoroshwa nje, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imeshindwa kuchunguza na kuchukua hatua.

Akichangia hotoba ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma bungeni mjini Dodoma jana, Bw. Mpina alisema Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inawajua watu hao kwa majina na kiasi cha pesa ambazo Watanzania wanamiliki katika benki ya nje.

“Iweje TAKUKURU haijatoa taarifa yoyote hadi sasa, hali hii inaleta mashaka kwa taasisi muhimu kama hii, kimsingi utoroshwaji mkubwa wa fedha za umma unapunguza akiba ya fedha za kigeni na kusababisha mfumuko wa bei.

“Utoroshwaji huu pia unapunguza ukusanyaji kodi pamoja na uwekezaji, fedha hizi zingeweza kutumika kwa manufaa ya Watanzania wote na kuchochea maendeleo,” alisema.

Alisema fedha hizo zingeweza kuboresha huduma za maji, afya, elimu, kilimo, miundombinu na kuongeza ukuaji uchumi ambapo Watanzania wengi wanateseka kutokana na umaskini walionao wakati fedha nyingi za umma zinaishia kwa watu wachache.

“Baadhi ya nchi ziliamua kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha fedha zilizotoroshwa na kuwekwa katika benki zilizopo nje ya nchi, zinataifishwa na kurejeshwa nchini mwao, nchi hizi ni pamoja na  Nigeria, Peru na Ufilipino.

“Benki ya dunia baada ya kuona sakata la wizi wa fedha za umma linaendelea siku hadi siku, iliamua kuanzisha mkakati maalumu wa kurejesha rasilimali zilizotoroshwa,” alisema Bw. Mpina.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mkanyageni Bw. Habib Mnyaa (CUF), alisema ripoti ya CAG ina dosari 13 ambazo zimechangia kukwamisha dhana ya utawala bora.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kutotekelezwa kwa mapendekezo ya ripoti hiyo ambapo dhana ya uwajibikaji kwa viongozi wa nchi ni kitendawili.

“Kwa mfano, Mbunge wa Monduli, Bw. Edward Lowassa, alichukua uamuzi wa kuwajibika katika nafasi yake jambo ambalo katika nchi inayojivunia utawala bora ni muhimu sana, viongozi wengi wametajwa katika ripoti ya CAG lakini hakuna hata mmoja ambaye amewajibika hadi walipoondelewa na Rais Jakaya Kikwete,” alisema Bw. Mnyaa.

No comments:

Post a Comment