04 July 2012

Kasoro zilizopo sekya ya kilimo ziondolewe sasa



NENO ‘Kilimo Kwanza’ ni kauli mbiu ambayo inawahamasisha wakulima nchini kuongeza juhudi kwenye kilimo cha kisasa ili kuingeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Rais Jakaya Kikwete ipo katika utekelezaji wa mpango huu wenye lengo la kuleta mapinduzi ya kijani katika sekta hiyo kiuchumi na kijamii.


Tangu kuanza kwa mpango huo, zipo kasoro nyingi zilizojitokeza ambazo zinastahili kutatuliwa mapema ili tusipoteza maana halisi na kushindwa kuleta mapinduzi yanayokusudiwa kwa mkulima.

Baadhi ya wadau wa kilimo, wamekuwa wakionesha wasiwasi wao wa kufanikiwa kwa mpango huo na kuleta mapinduzi ambayo yanakusudiwa kutokana na kasoro zilizopo.

Wadau wa kilimo wanasema,  bila kutatua kasoro zilizopo mpango huo hauwezi kufanikiwa kama inavyotarajiwa.

Sisi tunasema kuwa, Tanzania bado ina safari ndefu ili kufanikisha mpango huo. Dhamira na utashi katika mpango huo ni nzuri ili kuleta mapinduzi ya kilimo lakini vikwazo bado ni vingi.

Yawezekana mpango huo upo kisiasa zaidi, tatizo kubwa linaloweza kuufanya ukakwama ni ukosefu wa miundombinu kwa wakulima nchini. Miundombinu hiyo ni pamoja na barabara hasa ziendazo vijijini kwenye mazao ambazo hazipitiki kirahisi.

Hali hiyo inachangia pembejeo zishindwe kufika sokoni kwa wakati, baadhi ya viongozi serikalini na wataalamu wa kilimo, kushindwa kuwafikia wakulima vijijini na kuwapa elimu ya kilimo cha kisasa jambo linalochangia malengo ya mpango huo kukwama.

Kukosekana kwa soko la uhakika la mazao ya wakulima, huchangia mazao mengi kuharibika kabla ya kufika sokoni ili mkulima apate faida badala yake huingia hasara.

Jambo jingine linaloweza kukwamisha mpango huo ni baadhi ya wakulima kutofahamu mbinu za kisasa za uvunaji na uhifadhi wa mazao yao kabla ya kufikishwa sokono.

Imani yetu ni kwamba, ili mkulima apate mazao yenye kukubalika kwenye soko, wataalamu wa kilimo wanapaswa kuwa karibu na wakulima badala ya kukaa ofisini kama wanavyofanya sasa.

Wataalamu hao wanatakiwa kuwa karibu na wakulima ili kuwapa mbinu za kilimo bora cha mazao ya chakula, biashara na Serikali kuweka mpango maalumu wa kuboresha barabara.

No comments:

Post a Comment