11 July 2012
Temeke yatangulia nusu fainali Copa Coca-Cola
Na Janath Abdulrahimu
TIMU ya Temeke jana imeiliza Mji Magharibi kwa penalti 3-2 katika mechi ya robo fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola, iliyofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam baada ya kumaliza dakika 90 zikiwa sare ya bao 1-1.
Katika mechi hiyo iliyopigwa asubuhi, Mjini Magharibi ndiyo walioanza kupata bao dakika ya 79 lililofungwa na Salum Maulid wakati Abdul Hassan, aliisawazishia Temeke dakika ya 90.
Waliofunga penalti kwa upande wa Temeke ni Baraka Ntalukundo, Khalid Mwendakamo, Mohamed Dikougwa na Abdul Hassan wakati aliyekosa ni Anwar Kilemile.
Waliokosa kwa Mjini Magharibi ni Abdulrahman Mohamed na Salum Maulid, wakati waliofunga ni Alawi Kombo na Salum Shukuru.
Temeke itacheza na mshindi wa mechi ya robo fainali nyingine kati ya Kinondoni na Mwanza leo asubuhi kwenye uwanja huo huo.
Robo fainali ya pili ya michuano hiyo kati ya Mara na Morogoro, ilitarajiwa kuchezwa jana jioni kwenye uwanja huo huo.
Mechi zingine za robo zinaendelea leo, ambapo Dodoma itaumana na Tanga jioni na Kinondoni na Mwanza asubuhi.
Wakati huohuo, Kocha wa Temeke Edward Lazaro, akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, alisema ameyapokea vizuri matokeo hayo na anawashukuru wakazi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao.
Alisema atahakikisha anayafanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mechi hiyo, ili katika mechi ijayo yasijirudie tena.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment