02 July 2012

TBCC kuwanoa wajasiriamali Mwanza kumiliki viwanda leo


Na Mwandishi Wetu, Mwanza

IMEELEZWA kwamba mpango wa kuwajengea uwezo Watanzania wote namna ya kumiliki viwanda ikiwemo kutengeneza bidhaa zenye viwango bora umefikia katika hatua nzuri.

Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tanzania Business Creation Company Ltd (TBCC LTD), Bw. Elibariki Mchau mjini Mwanza wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mwendelezo wa semina za kuwajengea wajasiriamali uwezo wa kumiliki viwanda.

"Tanzania Business Creation tunatarajia kufanya semina kubwa katika miji ya Mwanza na Moshi katika mwezi huu wa saba, tarehe mbili hadi nne tutakuwa Aspen Hotel Mwanza na tarehe 16 hadi 17 tutafanya semina Moshi mkoani Kilimanjaro katika Hoteli ya Craine," alisema Bw. Mchau.

Alisema, katika semina hiyo watafundisha jinsi ya kumiliki viwanda na kutengeneza bidhaa mbalimbali zaidi 18 na wote watakaohudhuria semina hizo watatoka wakiwa na ujuzi wa kutengeneza bidhaa hizo.

"Na hivyo kumudu kuwa wamiliki wa viwanda, kwa kuanzia na viwanda vidogo vidogo, hivyo kujipatia ajira wao binafsi na kuajiri wengine na kujipatia kipato rasmi hatua ambayo itasaidia kuchangia uchumi wa taifa kwa njia hiyo," alisema.

"Sisi katika TBCC Ltd tunaamini kuwa wote wanaomiliki viwanda, wanamiliki uchumi. Tunawataka wakazi wa miji hiyo na wilaya jirani wafike katika semina hizo ili kwa pamoja tuweze kuinua uchumi wetu mmoja mmoja na wa taifa kwa ujumla," aliongeza Bw. Mchau.

Alisema, kigezo cha kuhudhuria semina nikujua kusoma na kuandika na umri ni kuanzia miaka 18 na kuendelea.

"Tangu tumeanza mpango huu mwaka 2009 mpaka sasa tumeshatoa ujuzi kwa watu zaidi ya 4,000 kwa nchi nzima. Tumeshafanya semina kama hizi Mbeya, Tanga, Arusha, Shinyanga, Kahama, Singida, Dodoma, Mbulu, Lushoto, Korogwe, Kilindi, Msata, Hanang, Mbozi, Geita, Moshi na Mwanza.

"Lengo letu hasa ni kuinua jamii ya wamiliki wa viwanda katika taifa letu na kutengeneza ajira za kutosha kwa taifa na hivyo kushirikiana na serikali katika kufikia azima ya kujitegemea kwani inawezekana kabisa ilimradi kuwa na maono sahihi kama haya," alifafanua Bw. Mchau.

Hata hivyo aliongeza kuwa katika semina hiyo washiriki watakutana na wataalamu mbalimabli waliobobea katika masuala ya uchumi nchini na wanaomiliki viwanda.
************
ANCHOR

CRDB yaziwezesha
SACCOS Manyara

Na Mary Margwe, Manyara

VYAMA vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) wilayani Mbulu Mkoa wa Manyara vimekopeshwa zaidi ya sh. milioni 280 kwa ajili ya kuendeleza shughuli mbalimbali za miradi zilizotolewa na Benki ya CRDB wilayani humo.

Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Bw.Isack Daudi Bayo wakati alipokua akiwasilisha taarifa  ya fursa za kupata mikopo kupitia benki mbalimbali katika kikao cha Baraza la Madiwani mjini hapa.

Bw. Bayo ambaye ni Diwani wa Kata ya Gehandu wilayani hapo alisema, benki hiyo ya CRDB hutoa mikopo kwa Saccos, ambayo inariba nafuu na isiyozidi asilimia 16 kwa mwaka ambapo ni maalum kwa Saccos.

“Hadi sasa benki hii imeidhinisha mikopo yenye thamani ya sh. milioni 280. kwa ajili ya Saccos ya Upendo Murray na Mbulu Teachers," alisema.

Bw. Bayo alisema hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu benki hiyo tayari imekwishatoa mikopo zaidi ya sh. milioni 180 kwa Saccos mbalimbali.

Alisema, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto tayari imekwishatoa mikopo kwa vijana yenye thamani ya sh. milioni 20.

Akizungumzia Benki ya NMB, Bw. Bayo alisema kuwa benki hiyo tayari imeshakutana na Saccos husika na wanaendelea na utaratibu mbalimbali za kupata mikopo hiyo ambapo aliongeza kuwa NMB nayo ni sawa na CRDB ambayo hutoa mikopo yake kupitia Saccos huku riba yake ikiwa asilimia 15 kwa mwaka.

Hata hivyo aliwataka wahusika kuweza kuhakikisha wanafuatia hali ya marejesho kikamilifu ili kuweza kuwapa imani benki zinazotoa fursa hizo kwa mikopo kwa wananchi wa wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment