'
Na Zahoro Mlanzi
KAIMU Kocha Mkuu wa timu ya Yanga, Fredy Felix 'Minziro', amekoshwa na kiwango kilichooneshwa na mchezaji wake, Athumani Idd 'Chuji' kwa kusema anarudi katika kiwango chake cha zamani.
Hayo aliyazungumza Dar es Salaam juzi wakati wa mechi ya kirafiki ya kimataifa kati yao na The Express ya Uganda, iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Katika mechi hiyo, mabao ya Yanga yalifungwa na Jeryson Tegete katika kipindi cha kwanza.
Minziro alisema,:"Nimefurahishwa na jinsi Chuji alivyocheza katika sehemu ya kiungo wa chini, amecheza kama nilivyomwambia, nina imani kama ataendelea kucheza hivi nitakuwa na kiungo mzuri sana kwa mwaka huu."
Alisema ana uwezo wa kupiga pasi ndefu zenye uhakika kitu ambacho viungo wengi hawana uwezo huo na kwamba atahakikisha anamuongezea mazoezi ili awe mwepesi zaidi.
Alisema pamoja na sifa hizo, Minziro alisema kiungo huyo hana budi kuwa mtulivu zaidi hasa anapovuka eneo la kati ya uwanja kwani inaonekana kutokuwa makini ila wakati yupo nyuma kuokoa anakuwa makini zaidi.
Timu hiyo inajiandaa na Kombe la Kagame linalotarajiwa kuanza Julai 14, mwaka huu ambapo yenyewe imepangwa na Atletico ya Burundi katika harakati za kutetea ubingwa wake.
No comments:
Post a Comment