23 July 2012

TANESCO yapata hasara mil. 15/- Pwani


Na John Gagarini, Kibaha

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), mkoani Pwani, linakadiriwa kupata hasara ya zaidi ya sh. milioni 15 kutokana na wezi wa huduma ya umeme.

Meneja wa TANESCO mkoani hapa, Mhandisi Jonson Mwigune, aliyasema hayo jana baada ya msako maalumu unaoendelea mkoani hapa nyumba hadi nyumba ili kubaini wezi wa umeme.


Alisema hadi sasa,  watu 10 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na makosa mbalimbali.

Aliongeza kuwa, waliokamatwa katika msako huo ni pamoja na wateja wanaojisambazia umeme na kusambaza kwa wengine kwa zaidi ya vyumba na vibanda sita wakitumia mita moja.

“Wizi mwingine ni ule wa kuchomoa nyaya za umeme kwenye mita na kuchezea mita ili zisisome, msako ulioanza Julai 15 mwaka huu, katika Wilaya za Kibaha na Kisarawe, watuhumiwa watashtakiwa kwa wizi na uhujumu shirika,” alisema Mhandisi Mwigune.

Aliwataka wananchi kuacha tabia za kuliibia shirika hilo kwani hatua kali zitachukuliwa kwa wote ambao watakamatwa na hawatafumbiwa macho ili iwe fundisho kwa wengine.

Ukaguzi huo ni endelevu ili kuwabaini watu wanaolihujumu shirika hilo na kusababisha hasara kubwa.

No comments:

Post a Comment