23 July 2012
Wazazi washauriwa kuwaepusha watoto kubakwa
Na Stella Aron
WITO umetolewa kwa wazazi na walezi nchini kuhakikisha watoto wao wa kike hawatembei ovyo hasa nyakati za usiku ili kuwaepusha na vitendo vya ubakaji ambavyo vinaonekana kushika kasi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa, idadi ya watoto wa kike wanaobakwa inaongezeka mara dufu.
Ofisa wa Kituo cha Mkono kwa Mkono (One Stop Centre), Bi. Ashura Mpatani, kinachoshughulika na wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia ukiwepo ubakaji katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, alisema wastani wa kesi sita za kubakwa watoto huripotiwa katika kituo hicho kila siku wakati wa mfungo wa Ramadhani ukilinganisha na watoto wanaobakwa miezi mingine.
Bi. Mpatani alitaja mambo yanayochangia ongezeko la vitendo vya ubakaji kwa watoto kuwa ni pamoja na wazazi kuwaacha watoto watembee wenyewe nyakati za usiku na kusababisha watu waovu kutumia mwanya huo kutimiza matakwa yao.
“Kibaya zaidi, wazazi ambao hutumia vilevi huchelewa kugundua kama watoto wao wamebakwa hivyo kuwaweka katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali ukiwemo UKIMWI.
“Vitendo hivi vya ubakaji, vinaongezeka kutokana na wahusika kutochukuliwa hatua za kisheria kwa sababu mbalimbali moja wapo ni kukosekana ushahidi au kuupoteza,” alisema.
Alisema madaktari wanasema mtu anayefanyiwa kitendo anatakiwa kutooga, kunawa hivyo anapaswa kwenda polisi kuandika maelezo, kuchukua PF3 na kwenda hospitali kupimwa ili kutunza ushahidi na kupata dawa.
Utafiti uliofanywa na TAMWA, Zanzibar Aprili mwaka huu, umeonesha mwaka 2011, kesi zipatazo 400 za ubakaji ziliripotiwa visiwani humo.
Pia utafiti huo ulibaini sababu za watoto wengi kubakwa ni pamoja na wazee (wazazi au walezi), kutofuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment