30 July 2012
TAMWA: Waliokufa Mv Skagit wengi wao ni wanawake, watoto
Na Stella Aron
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini (TAMWA), kimeitaka Serikali kuweka mikakati ya kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri baharini ili kuepusha vifo visivyo vya lazima kwani waathirika wakubwa wa ajali zinazotokea ni wanawake na watoto.
Taarifa ya iliyotolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa TAMWA, Bi. Ananilea Nkya, ilisema kati ya watu 105 ambao wameopolewa wakiwa wamekufa katika ajali ya Mv Skagit, iliyozama hivi karibuni, wanawake walikuwa 45, watoto 19.
Alisema watu wengine zaidi ya 50 wanaosadikiwa kufa katika ajali hiyo, hawajapatikan kabisa.
Bi. Khadija Ali, mkazi wa Fuoni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, alidai kumpoteza binti yake katika ajali hiyoambaye alikuwa akisoma kwenye Chuo Kikuu cha Kiislamu, mkoani Morogoro.
Alisema ili kuepusha ajali za vyombo vya usafiri wa bahari, lazima Serikali iweke mikakati madhubuti ili kuthibiti usajili wa vyombo hivyo kwani hali ilivyo sasa, meli zinaruhusiwa kufanya kazi zikiwa chini ya viwango na kukosa mfumo imara wa kujihami wakati wa dharura.
“Binti yangu alikuwa akirejea nyumbani akitokea chuoni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein inapaswa kuhakikisha Serikali yake na ile ya Muungano zinaangalia namna bora ya kushughulikia vyombo hivi,” alisema Bi. Ali.
Septemba 2011, meli nyingine Mv Spice Islander ilizama baharini wakati ikitoka Unguja kwenda Pemba na kuua watu zaidi ya watu 1,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
TAMWA imetoa pole kwa familia zote zilizopoteza ndugu zao kutokana na ajali hizo na kuitaka Serikali ihakikishe familia hizo zinalipwa fidia na wote waliohusika na ajali hizo kwa namna moja au nyingine, wanafikishwa katika vyombo vya sheria.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment