30 July 2012
TIPF yawataka Waislamu kushiriki sensa ya watu, makazi
Na Anneth Kagenda
TAASISI ya Tanzania Islamic Peace Foundation (TIPF), imewataka Waislamu nchini kuwapuuza watu wanaotaka kukwamisha ushiriki wao katika Sensa ya Watu na Makazi badala yake washiriki kikamilifu kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Shekhe Sadick Godigodi, alisema wapo baadhi ya watu wanaowashawishi Waislam kutoshiriki sensa na kutaka wapuuzwe kwani dhamira ya Serikali ni kupanga mipango ya maendeleo.
“Sisi TIPF tunaunga mkono tamko la Shekhe Mkuu, Mufti Issa Bin Shaaban Simba, linalotutaka Waislamu washiriki sensa kwani yeye ndio kiongozi na msemaji wetu,” alisema Shekhe Godigodi.
Alisema wao wataendelea kumsikiliza Mufti Simba na wale ambao wanasema kiongozi huyo si msemaji, wajitokeze na kusema msemaji ni nani, amechaguliwa na akina nani, lini na mkutano upi.
Aliongeza kuwa, hoja zinazotolewa na kikundi kimoja (hakukitaja), ambacho kinaitaka Serikali iingize kipengele cha dini katika fomu za sensa haina mashiko na kusisitiza kuwa, Watanzania wote ni sawa na sensa inafanyika kwa maendeleo ya wananchi wote si dini fulani.
Shekhe Godigodi alisema kinachotakiwa kwa Watanzania wote bila kujali dini zao ni kuwa na mshikamano na kuwapuuza watu wanaotaka kukwamisha mambo ya maendeleo.
“Kikundi hiki mara nyingi kimekuwa kikiendesha propaganda za kuonesha Serikali haiwapendi na kulisikiliza Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), jambo ambalo si kweli.
“Taasisi yao imesajiliwa na Serikali ambayo ndio imewapa kibali cha kufungua redio na televisheni, sasa kama haipendwi vibali vya kufanya shughuli zao wamevipata wapi,” alisema.
Alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa niaba ya taasisi hiyo kutokana na hotuba nzuri aliyoitoa mkoani Mbeya hivi karibuni na kusisitiza kuwa, suala la dini ya Mtanzania halitaingizwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi.
Alisema lengo la sensa ni kujua idadi ya Watanzania ili Serikali iweze kupanga mipango ya maendeleo ambayo haipangwi kwa misingi ya dini yoyote.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment