31 July 2012

TAFF wapewa changamoto



Na Elizabeth Mayemba

SHIRIKISHO la Filamu Tanzania (TAFF), limetakiwa liendelezwe na watu wa tasnia
hiyo, ili serikali iweze kutia mkono wake.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa semina hiyo iliyoandaliwa na TAFF, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Utamaduni na Michezo ambaye alikuwa ni
mmoja wa wakufunzi wa semina hiyo, Profesa Eliasante Gabriel alisema maendeleo ya
tasnia ya filamu lazima yaanzishwe na wenyewe, ili serikali iweze kutia mkono wake.


"TAFF inatakiwa ijenge imani kwanza na wadau wake na pia maendeleo ya tasnia
hiyo, lazima yaanzishwe na tasnia hiyo ili serikali iweze kutia mkono wake," alisema
Profesa Gabriel.

Alisema pia TAFF iwe na kikundi cha watu wanaojua kufikiria si kuwa na watu ambao hawajui kufikiri ya mbele na kwamba serikali itahakikisha itakuwa bega kwa
bega na wasanii nchini katika kulinda kazi zao.

Profesa Gabriel alisema pia Shirikisho hilo la filamu nchini, linatakiwa kuwa na
changamoto kubwa ili kuhakikisha haliwi kama chama cha siasa na endapo tasnia
hiyo itaepuka hilo basi itakuwa imepiga hatua kubwa.

Aliongeza kuwa TAFF iwe kwa ajili ya baadaye na anaimani waliobuni kitu
hicho, hawana nia ya kutaka kufaidika kwa sasa bali ni kwa ajili ya wasanii wa kizazi
kijacho.

"Kuna wengine wakibuni kitu, cha kwanza wanajifikiria wao tu lakini si kwa baadaye,
ila TAFF inaonekana kabisa watakaofaidika ni wengine na hivyo ndivyo inavyotakiwa," alisema.

Pia Profesa huyo alisema endapo serikali itafanikiwa kudhibiti kazi za wasanii,
wizara yake kupitia tasnia hiyo inaweza kuingiza katika bajeti yake sh. bilioni 16 hata kwa  mwezi.

No comments:

Post a Comment