31 July 2012

BFT yahuzunishwa Kidunda kudundwa


Na Mwali Ibrahim

SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) limehuzunishwa na bondia wake, Selemani Kidunda aliyepigwa katika mashindano ya Olimpiki yanayoendelea London, Uingereza.

Bondia huyo pekee wa Tanzania, juzi alichezea kichapo kwa kupigwa kwa pointi 20-7 na bondia kutoka Moldova Belous Vasilii,.


Kidunda ndiye aliyekuwa akitoa matumaini kwa Watanzania wengi, ambao waliamini angeweza kuwakilisha vyema na kuleta medali miongoni mwa wachezaji wengine waliokwenda katika mashindano hayo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga alisema Kidunda alijitahidi lakini mpinzani wake alionekana kumzidi uwezo kwa mujibu wa kocha wake, Remmy Ngabo hivyo kushindwa kujibu mashambulizi ipasavyo.

"Tumeyapokea matokeo kama yalivyo, lakini tumesikitika mno kwani tuliamini angeweza kuleta medali kwa kiasi kikubwa kwani maandalizi aliyoyapata yalikuwa ni mazuri, lakini mpinzani wake anaonekana alikuwa amejiandaa vyema zaidi na yote ni matokeo," alisema.

No comments:

Post a Comment