18 July 2012
Simanzi maziko ya waliokufa ajalini Geita
Na Faida Muyomba, Geita
SIMANZI na vilio juzi vilitawala katika ibada ya ibada ya wanafamilia wanne waliokufa katika ajali ya mabasi madogo ya abiria maalufu kama michomoko, iliyotokea wilayani Geita.
Wanafamilia hao ni Eliud Ngovongo (36) na wanawe watatu ambao ni Emison (7), Amin (10) na Sara (4) ambapo katika ajali hiyo, watu 11 walikufa papo hapo na 12 kujeruhiwa vibaya.
Ajali hiyo ilihusisha gari lenye namba T 344 AZE na T 421 BHS ambayo yalikuwa yakifanya biashara ya kubeba abiria kutoka Geita kwenda Katoro ambapo miili hiyo ilisafirishwa kwenda wilayani Kibondo, mkoani Kigoma kwa maziko.
Kutokana na ajali hiyo ambayo imewagusa watu wengi wilayani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Bw. Magalula Magalula, ameliagiza Jeshi la polisi kuhakikisha magari hayo 'michomoko', hayafanyi biashara ya kubeba abiria na wale ambao watakiuka agizo hilo, wakamatwe na kuchukuliwa hatua.
Akizungumza na wamiliki pamoja na madereva wa magari hayo mjini hapa jana, Bw. Magalula ambaye alikuwa ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, alisema madereva wa magari hayo hawafuati sheria za usalama barabani badala yake wanajali pesa si vinginevyo.
“RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa), naagiza tena, magari haya yasimame mara moja kubeba abiria, hatuwezi kuangalia watu wakiendelea kufa kwa uzembe wa wachache, lazima tulinde usalama wao kama Serikali, huu ndio msimamo wangu magari yenu yatumike kwa kazi nyingine si kusafirisha abiria.
“Haya magari yana uwezo wa kubeba abiria watano lakini yamekuwa yakibeba kati ya 14 na 16, pamoja na mizigo, mwendo wake si mzuri na yanakiuka sheria za usalama,” alisema.
Bw. Magalula alitumia mwanya huo kutuma salamu kwa waendesha pikipiki zinazobeba abiria na kusisitiza kuwa, dawa yao iko jikoni kama na wao watashindwa kufuata sheria za usalma barabarani.
Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi Mamlaka ya Udhibiti na Usafirishaji Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), mkoani Mwanza, Bw. Alfred Waryana, alisema mamlaka hiyo tayari imesitisha kutoa leseni za magari hayo tangu Juni 30 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva hao, Bw. Emmanuel Bilamba, alimuomba Bw. Magalula kuwapa miezi mitatu ya kuendelea na biashara hiyo ili waweze kuendesha familia zao.
Alisema kusitishwa utoaji wa huduma hiyo, kunaweza kuchangia wimbi la ujambazi wilayani hapa kutokana na vijana wengi kutokuwa na ajira lakini ombi lao lilikataliwa.
Kutokana na hali hiyo, madereva hao walilazimia kufunga Barabara Kuu kuzuia magari yasipite ili kushinikiza waruhusiwe kubeba abiria katika muda huo.
Akizungumza katika ibada ya kuaga miili ya marehemu iliyofanyika kwenye Kanisa la Anglikana, Askofu Mkuu wa Kanisa la African Inland (AICT), Musa Magwesela, alisema vifo hivyo si mpango wa Mungu bali vimetokana na baadhi ya watu kutotii sheria.
“Kutokana na vifo hivi hatupaswi kumlaumu Mungu, tujilaumu sisi wenyewe kwani baadhi ya madereva wanaendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa pombe na dawa za kulevya.
Mchungaji wa Kanisa la Anglikana, Mathias Mwebesa, alimpongeza Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Magalula kwa hatua alizochukua baada ya ajali hiyo kutokea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment