19 July 2012
Shahidi adai waliishi nchini Yemen kama ombaomba
Na Rehema Mohamed
SHAHIDI wa tatu katika kesi ya biashara haramu ya kusafirisha binadamu Bw. Abdulswamadu Omary (30), jana ameieleza Mahakama ya Hahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kuwa aliishi nchini Yemeni na wenzake kama ombaomba.
Kesi hiyo inamkabili mfanyabiashara wa jijini Arusha, Bw.Salim Ally, ambaye anadaiwa kuwasafirisha Bw. Abduswamad Zakaria, Bw. Hamidu Biabato, Bw. Raufu Biabato na Bw. Sadick Almas Kutoka Mwanza kwenda nchini humo kinyume cha sheria.
Bw. Omary aliyasema hayo wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Ilvin Mugeta, huku akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa wa Serikali Bw. Prospar Mwangamila.
Huku akitokwa na machozi, Bw. Omaey alidai hali hiyo ilitokana na kukosa msaada wa chakula na malazi kutoka kwa mshtakiwa Bw. Ally ambaye ndiye aliyewapeleka nchini humo kwa ajili ya kumfanyia shughuli za ujenzi.
Alidai kuwa, hali hiyo iliwalazimu kwenda baharini kufanya kazi za kubeba Pweza wa wavuvi na kuwapeleka katika mizani kupimwa ili waweze kupata fedha za kujikimu na walilipwa Liyal 20.
“Baada ya siku kadhaa, wote tulipata maradhi ya upele na kifua, ilibidi tuuze vifaa vyetu vya ujenzi ili tuweze kununua dawa lakini fedha hazikutosha,” alisema.
Alidai kuwa, walipona maradhi hayo baada ya kupata msaada wa kupelekwa hospitali kutoka kwa mama wa kijana aliyemtaja kwa jina la Bw. Mohamed Ally ambaye ni ukoo mmoja na mshtakiwa.
Bw. Omary alisema aliwahi kuvamiwa na kupigwa hadi kuvuliwa nguo na vibarua waliokuwa wakijenga nao jengo la mshtakiwa la gholofa tatu wakimdai ujura wa kazi walizokuwa wakizifanya.
“Wakati tunafanya kazi ya ujenzi, Bw. Ally alikuwa akituma fedha pungufu ili niwalipe vibarua ambao wengine walikuwa wanakosa fedha hivyo kunivamia, kunipiga na kunichania nguo,” alisema.
Kesi hiyo itaendelea tena leo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment